October 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TPA: Ujenzi wa bandari mpya ya Mbamba Bay kuleta ajira, kukuza uchumi

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari hapa nchini (TPA) imesema kuwa ujenzi wa bandari mpya ya kisasa wa Mbamba Bay unaogharimu kiasi cha bilioni 75.8 ni mradi mkubwa wa kimkakati ambao utaleta manufaa makubwa kwa taifa wakati wa ujenzi na hata baada ya kukamilika kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kukagua eneo itakayojengwa bandari hiyo katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, Naibu Mkurugenzi wa TPA, Juma Kijavara amesema miongoni mwa faida kubwa za ujenzi wa bandari hiyo ni upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa eneo la mradi na maeneo ya jirani, hususan vijana ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa familia na wilaya hiyo kwa ujumla.

Pia amesema kuwa fursa za biashara mbalimbali zitaongezeka kwa wananchi wa eneo hilo kupitia utoaji wa huduma kwa mkandarasi pamoja na wafanyakazi wa mradi.

“Hii itaongeza kipato kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati wakati wa utekelezaji wa mradi huu wa miaka miwili,” alisema Kijavara na kuongeza kuwa faida nyingine ni ujenzi wa miundombinu saidizi kama vile barabara, maji na umeme zikiwa ni faida zaidi kwa wananchi wa eneo hilo.

Pia amesema bandari hiyo itakuza uchumi wa Tanzania na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia na kuhamasisha uwekezaji zaidi kwa sekta binafsi na umma, hususan katika sekta ya viwanda, usafirishaji, biashara  na utalii uliopo katika maeneo ya Ziwa Nyasa ambao ni muhimu kwa uchumi wa taifa letu.

Aidha, Waziri Mbarawa aliipongeza TPA kwa utekelezaji wa mradi huo mkubwa na utendaji kazi mzuri wenye tija kwa taifa.

“Bandari hii ya kisasa itapunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani, hususan madini, mazao ya kilimo na uvuvi kwa kuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa na kupelekea gharama za usafirishaji kupungua na kuleta unafuu wa bei kwa wananchi,” amesema Waziri Mbarawa.

“Juzi juzi tu tumezindua mradi mwingine mkubwa wa ujenzi wa matanki yenye ujazo mkubwa kwa ajili ya kuhifadhia mafuta kwenye bandari ya Dar es Salaam. Sasa tumezindua ujenzi wa bandari hii ili kuifungua nchi na fursa mbalimbali ikiwemo ajira kwa Watanzania.

“Hizi ni juhudi kubwa sana na naipongeza sana TPA kwa utekelezaji wa miradi hii mbalimbali inayofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan yenyemalengo ya kukuza uchumi na kufungua fursa za biashara kwa Watanzania,” amesema.

Ujenzi wa bandari hii unahusisha pamoja na maeneo mengine, ujenzi wa gati mbili zenye urefu wa mita 103 zenye uwezo wa kuhudumia meli mbili kubwa, tofauti na uwezo wa bandari ya sasa ambayo inahudumia zaidi boti ndogo za kubeba mizigo na abiria.

Pia utahusisha ujenzi wa maghala, nyumba za watumishi, jengo la utawala, jengo la abiria, karakana, mnara wa tanki la maji, jengo la huduma za afya, daraja lenye urefu wa mita 105 na upana wa mita 15 kwa ajili ya magari ya kubebea mizigo, eneo la kuhifadhia makontena 3,000 ya mizigo, barabara za ndani na nje ya bandari kwa ajili ya magari kuingia na kutoka bandarini hapo.

Awali, Mhandisi wa mradi huo kutoka TPA John Paul amesema kuwa TPA imeshamlipa mkandarasi mjenzi malipo ya awali kiasi cha Sh bilioni  3.2 sawa na asilimia 5 na kumlipa Mhandisi Mshauri kiasi cha Sh milioni 448.1 kama malipo ya awali ambayo ni sawa na asilimia 10.

About The Author