September 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rais Samia aanza ziara Ruvuma leo

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, leo Jumatatu anaanza ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma  Jumatatu ambayo ataihitimisha siku ya tarehe 28 mwezi huu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Ahmed Abbas Ahmed,  aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Samia akiwa mkoani humo atafanya mambo makubwa matatu ambayo ni kufunga tamasha la tatu la taifa la utamaduni linalomalizika leo na kufanya ziara ya kikazi kuanzia kesho tarehe 24 mpaka 28.

Alisema Rais atazitembelea wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma ambapo ataongea na wananchi wa Mkoa huo kupitia mikutano ya hadhara na atazindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya mandeleo iliyoko mkoani humo.

RC alisema Rais Samia pia atashiriki mkutano wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi CCM Taifa litakalofanyika wilayani Songea na atafunga kikao hicho tarehe 28 Septemba na kuhitimisha ziara yake siku hiyo ambayo pia ataongea na wananchi katika uwanja wa Majimaji.

“Nawakaribisha wananchi waje kwenye mkutano wa tarehe 28 atakapohitimisha ziara yake na nawakaribisha waandishi wote wa habari kwa namna ya kipekee washiriki ziara ya mheshimiwa Rais kuanzia mwanzo mpaka mwisho na siku atakapoondoka mkoani hapa tarehe 29 tujitokeze kumshangikiwa kwa ziara yake,” alisema

Wakati huo huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Pindi Chana alizungumza na machifu wa mkoa wa Ruvuma na kuwataka kuendeleza mila na utamaduni kwa kuwarithisha kizazi cha sasa na kizazi kijacho.

Aliwaambia machifu hao kuwa Tanzania inautulivu na amani kutokana na kazi kubwa inayofanywa na viongozi wa dini na machifu wa makabila mbalimbali.

“Mila na desturi muendeleze, leo hii nchi yetu watu hawaulizani dini wala kabila na hiyo ni kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa dini na machifu kwa hiyo mnawajibu wa kuendeleza kurithisha,” alisema

About The Author