December 26, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tamasha la utamaduni kitaifa lafunguliwa Songea

 

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro amewaasa watanzania kuzingatia miiko, mila na desturi za kitanzania na kuwarithisha watoto na vijana ili kujiepusha na tamaduni za kigeni zisizofaa kwa jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).

Aidha, ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwachukulia hatua kali wale wale wanaoua mila na desturi za watanzania kwenye mitandao ya kijamii.

Akizindua Tamasha la tatu la Utamaduni Kitaifa kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea, alisema kusipokuwa na utamaduni hakutakuwa na utu na wasipouenzi hawatauendeleza.

“Ili Taifa liwe hai lazima tuenzi na kuendeleza utamaduni wetu, na lazima turithishe utamaduni wetu kwa vijana na watoto na lazima tuwafundishe watoto wetu mil ana desturi za kitanzania, Kiswahili tuwafundishe miiko mbalimbali na historia yetu kwa kuwa hawa watoto ni taifa la kesho,”alisema.

Alisema katika maadhimisho ya tamasha hilo ilitolewa semina ya maadili na utamaduni iliyofundisha jinsi ya kuenzi utamaduni na namna ya kukabiliana na madhara ya sayansi na teknolojia katika kulinda, kuenzi na kuendeleza mil ana desturi.

“Sasa hivi duniani kuna suala linaitwa haki za binadamu ni jambo linalopaswa kuliheshimu na kulizingatia lakini tusitumie haki za binadamu kuingiza tamaduni za kigeni zisizofaa katika jamii yetu,”alisema.

“Taasisi za elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu ni muhimu kurithisha utamaduni wetu una mila zetu katika kupambana na mmonyoko wa maadili,”alisema.

Alikemea tabia ya familia kulaumu mmonyoko wa maadili badala ya kujikita kutoa elimu kwa watoto na vijana ili kuishi kwenye tamaduni za mtanzania.

Hata hivyo, alisema taasisi za dini zina nafasi ya kukabiliana na mmonyoko wa maadili na kurithisha utamaduni kwa watoto na vijana.

“Tuwafundishe maadili mema watoto wetu, viongozi wa dini mna kazi kubwa sana na maadili mengi ya dini yanatusaidia kulinda tamaduni zetu,”alisema.

Awali, Dk.Ndumbaro alibainisha kuwa Septemba 8, 2021 katika maadhimisho ya utamaduni Bujora mkoani Mwanza Rais Samia Hassan Suluhu alitoa maelekezo kwa Wizara hiyo kuandaa tamasha la kitaifa litakalofanyika kila mkoa.

“Maelekezo yale yametufanya tuwe Songea leo, uwepo wetu hapa ni maelekezo ya Rais Samia kudumisha tamaduni zetu, ”alisema.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na makabila zaidi ya 120 na lugha za kijamii zaidi ya 150 na ni utajiri wa kiutamaduni.

“Utamaduni wetu unategemea nguzo zifuatazo moja ni upendo, mshikamano, umoja, amani na utulivu, yote tunayoyafanya ili kuendeleza nguzo hizi,”alisema.

About The Author

error: Content is protected !!