KUELEKEA pambano la marudiano raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2024/25), dhidi ya CBE ya Ethiopia, mabingwa wa Tanzania, Yanga wameitambulisha Benki ya NMB kuwa ni mmoja wa wadhamini wa mechi hiyo, ushirikiano uliopewa jina la ‘Timu Bora, Benki Bora’. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Yanga wanashuka dimbani Jumamosi ya Juni 21 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuumana na Wahabeshi hao, wakiwa na uongozi wa bao 1-0 walioupata katika mechi ya kwanza jijini Addis Ababa, Ethiopia na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya utambulisho wa wadhamini wa mechi hiyo, Meneja Biashara wa NMB Zanzibar, Naima Said Shaame, alisema siri ya uamuzi wao wa kujitosa kuidhamini Yanga ni mvuto ilionao klabu hiyo, unaoakisi mafanikio makubwa katika soka kitaifa na kimataifa.
“Tumevutiwa na mafanikio ya klabu hii, tukaona ipo haja ya Timu Bora kupewa nguvu na Benki Bora. Wametoka kutwaa Ngao ya Jamii katika ufunguzi wa msimu huu, lakini katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wamefuzu raundi hii kwa kishindo baada ya kuwachapa Vital’O ya Burundi kwa jumla ya mabao 10-0.
“Kwa kutambua ukubwa wa Yanga, tukalinganisha na ukubwa wa NMB, tukaona ipo haja ya kuwasapoti katika mechi dhidi ya CBE itakayopigwa hapa wikiendi hii na leo tuko hapa kutambulishwa rasmi washirika wa Yanga kuelekea mechi ya CBE,” alisema Naima.
Alibainisha ya kwamba, ushirikiano baina ya benki yake na Yanga umeshaanza katika kuanikiza wiki nzima na wanaamini mchango wa taasisi yake utakuwa chachu ya Yanga kushinda mechi hiyo na kufuzu hatua ya makundi kwa mara ta tatu katika historia yao.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha mashabiki wa Yanga kuwa, huu sio mwanzao, kwani tunafanya kazi na Yanga katika maeneo mbalimbai ikiwemo usajili wa wanachama kupitia kadi tofauti tofauti. Ukiona Tawi la NMB, maana yake umeiona Yanga na unaweza kusajili uanachama wako hapo.
“Ili kuipa Yanga ubora na ukubwa inaostahili, mashabiki wajitokeze kurasmisha ushabiki wao kuwa uanachama kwa faida ya timu yao. NMB Zanzibar tunashukuru mechi hii kuletwa hapa, tukiamini itaongeza idadi ya mashabiki wa Yanga watakaojisajili kwa wanachama,” aliongeza.
Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Shaaban Kamwe, aliwashukuru NMB na wadhamini wenza kwa kuchagua kushirikiana na timu yake katika kuipa nguvu kuelekea hatua ya makundi CAF CL.
“Tunawashukuu NMB na wadhamini wengine wote waliowezesha wiki hii yote ya kujiandaa kuelekea mechi hiyo, mmeiheshimisha Yanga, kwani kabla hatujahesabu mauzo ya tiketi zetu za mechi, tayari tushaingiza zaidi ya Sh. Mil. 200 kutoka kwa wadhamini wetu hawa tu,” alitamba Kamwe.
Alibainisha ya kwamba ratiba ya matukio kwa Ijumaa hii yatafunguliwa kwa dua maalum itakayosomwa katika Madrassat Swifatul Nnabawwiyah iliyopo Kilimani kwa Msolopa, Zanzibar asubuhi na baada ya Swala ya Ijumaa, watatoa misaada kwa Watoto Yatima visiwani hapa.
“Tayari kikosi chetu chote kimetua Zanzibar kasoro Farid Mussa Maliki tu ambaye ni majeruhi na sababu za kusafiri na kikosi chote ni kundelea kujiandaa na mehi za ligi kuu zinazofuata, tuna ratiba ngumu mno ambayo hairuhusu mchezaji yeyote kuachwa mbali na kikosi.
“Tukimalizana na CBE, tutarejea katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambako tutaumana na Ken Gold ya Mbeya kule nyumbani kwao, kisha tutawafuata KMC ya Kinondoni Dar es Salaam na baadaye kuivaa Pamba Jiji ya Mwanza,” alifafanua Ali Kamwe.
Ukiondoa NMB, Wadhamini wengine wa mechi ya Yanga dhidi ya CBE SA ni Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la Bima Zanzibar, Inuka Fund, PBZ, ZIPA, wanaoungana na wadhamini wengine wa Yanga kama GSM, SportPesa na Azam Tv.
ZINAZOFANANA
Black Gold kasino mambo iko huku
Meridianbet yatoa msaada wa jezi Kimara
Piga mshindo wa maana na Meridianbet leo