October 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yaahidi kuboresha mashindano ya Gofu

 

MASHINDANO ya siku tatu ya Gofu ya Tanzania Ladies Open Golf Tournament yamehitimswa mwishoni mwa wiki jijini Arusha huku wadhamini wakuu wa mashindano hayo, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wakiahidi kuendelea kuyaboresha zaidi mashindano hayo ili kuyoangozea ubora na ushindani utakaowavutia zaidi washiriki kutoka ndani na nje ya nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Mashindano hayo ya siku tatu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Klabu ya Gofu ya Gymkhana jijini Arusha yalifanikiwa kuvutia washiriki kutoka vilabu vyote vya mchezo huo hapa nchini sambamba na washiriki wengine kutoka katika mataifa ya Kenya na Uganda. Mchezaji Mercy Nyanchama kutoka nchini Kenya alifanikiwa kuibuka mshindi wa jumla wa mashindano hayo.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa washindi mbalimbali wa mashindano hayo, Meneja Mahusiano wa Benki ya NBC, Gerald Tarimo pamoja na kuwapongeza washiriki pamoja na washindi mbalimbali wa mashindano hayo alisema  benki hiyo itaendelea kuyaunga mkono ikiwemo kuyaboresha zaidi ikiwa ni sehemu ya jitihada zake katika kuchochea ushiriki wa wanawake katika michezo.

“Pamoja na kuvutiwa na idadi kubwa ya washiriki kwenye mashindano haya, zaidi tumevutiwa na maandalizi mazuri yaliyochochea ushindani uliokusudiwa kwa kuwa washiriki hawakuwa na changamoto ambazo zingeweza kuathiri uwezo wao kimchezo.’’

“Mara nyingi NBC tumekuwa tukikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi wa kiume vikiwemo vilabu vya mpira wa miguu kwenye ligi tatu tunazozidhamini nchini ikiwemo Ligi Kuu ya NBC, hivyo tunapopata nafasi ya kufurahia na kukabidhi zawadi kwa washindi wanawake kama leo hivi kwetu ni furaha pia,’’ alisema.

Kwa mujibu wa Tarimo, kufuatia mafanikio yanayoendelea kuonekana kupitia udhamini wa benki hiyo kwenye mchezo wa gofu nchini, benki ya NBC inadhamiria kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa mchezo huo kufanikisha mashindano mbalimbali kwa viwango vyenye ubora zaidi ili kuchochea ukuaji na kuibua vipaji vipya vya mchezo huo wakiwemo watoto.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU), Queen Seraki pamoja na kuwapongeza washiriki na washindi mbalimbali wa mashindano hayo wakiwemo wale waliotoka nje ya nchi, pia aliwashukuru wadau mbalimbali waliofanikisha mashindano akiwemo mdhamini mkuu wa mashindano hayo Benki ya NBC.

Aidha, Seraki, alitoa wito kwa jamii hususani wanawake kushiriki kwa wingi kwenye mchezo huo unaojiongezea umaarufu hapa nchini huku akiwasii wapuuzie dhana iliyojengeka kwa muda mrefu kuwa mchezo wa gofu ni mahususi tu kwa watu wenye kipato kikubwa kwenye jamii au wanaume tu.

“Maandalizi mazuri yaliyohusisha pia zawadi nzuri na zenye viwango kama ilivyokuwa kwenye mashindani haya ndio chachu ya kuendelea kuvutia zaidi washiriki kutoka ndani na nje ya nchi na kwenye hilo tunawashukuru sana wadhamini wetu hususani benki ya NBC.

“Ni matumaini yetu wataendelea kutuunga mkono zaidi mashindano yajayo kwa kuwa tunatazamia kuwa na mambo mazuri zaidi kutokana na mwamko mkubwa unaoendelea kushuhudiwa ukihusisha ongezeko kubwa la wachezaji na vipaji vipya vya mchezo huu,’’ alisema.

About The Author