December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Benki ya Exim yahitimisha kampeni ya “Tap Tap Utoboe’’ kwa mafanikio

 

BENKI ya Exim Tanzania imehitimisha rasmi kwa mafanikio kampeni yake ya Kidijitali ya miezi mitatu iliyojulikana kama Tap Tap Utoboe, huku ikitangaza washindi wa droo kuu ya mwisho, waliojishindia zawadi ambazo ni gari jipya aina ya Mazda CX-5 kwa mshindi wa kwanza, Bajaj aina ya TVS kwa mshindi wa pili na pikipiki aina ya boxer BMX kwa mshindi wa tatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Lengo la kampeni hii ilikuwa ni kuhamasisha wateja wa benki ya Exim kufanya miamala yao kwa kutumia simu zao za mkononi na kupitia mtandaoni.

Washindi hao Geofrey Muganyizi, Irene Dominick na Bhavesh Gorecha walipatikana kupitia droo kubwa ya mwisho iliyofanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam mapema hii leo chini ya usisamizi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania.

Akizungumza mara baada ya kutangazwa kwa washindi hao Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Biashara za Kati wa Benki ya Exim Tanzania, Andrew Lyimo alisema tangu kuanza kwa kampeni hii mwezi Juni, zaidi ya wateja 200 wameshinda zawadi za fedha taslimu ambapo washindi 10 kila wiki walipata zawadi ya Sh. 50,000 huku washindi 10 kila mwezi wakipata  zawadi ya Sh. 100,000 kwa kipindi chote cha kampeni hii.

“Nitumie fursa hii kuwapongeza washindi wetu wote waliotangulia na zaidi pia niwapongeze washindi wa droo yetu kubwa tuliyoifanya hii leo.  Kama tulivyobainisha hapo awali Bw Geofrey Muganyizi ambaye ni mshindi wa kwanza atapata gari jipya aina ya Mazda Cx 5 ambapo itakuwa imwekwa mafuta full tank pamoja na bima kubwa ya mwaka mzima buree. Mshindi wa pili, Irene Dominick yeye atapata Bajaj aina ya TVS, na mshindi wa tatu Bhavesh Gorecha atapata pikipiki aina ya Boxer BMX. Zote zikiwa na mafuta pamoja na bima kubwa kwa mwaka mzima’’ alisema.

Akizungumzia zaidi mafanikio ya kampeni hiyo, Stanley Kafu, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim, alisema: “Kampeni ya Tap Tap Utoboe imekuwa na matokeo mazuri katika kuongeza uelewa na matumizi ya huduma zetu za kidijitali. Tumefurahi kuwa wateja wetu wengi wamevutiwa na huduma hii na hili limedhihilishwa na ongezeko la miamala ya kidijitali tangu kampeni hii ianze mpaka sasa hivi”.

“Dhumuni kuu ni kuhakikisha mteja wetu anapata huduma zenye ubora, kwa wakati popote alipo  kwa gharama nafuu,” aliongeza Stanley.

Naye Silas Matoi, Mkuu wa Njia Mbadala za Kidijitali wa Exim Bank, alielezea umuhimu wa ubunifu wa kidijitali kwa benki hiyo, alisema ubunifu wa kidijitali ndio kiini cha mkakati wetu wa kuboresha huduma zetu kwa wateja.

“Kampeni ya Tap Tap Utoboe imeonesha jinsi teknolojia inavyoweza kubadilisha namna ambavyo wateja wetu wanatumia huduma za kifedha. Tumewavutia wateja wapya na wa zamani kwa kuwapa fursa ya kushinda zawadi, huku tukiunga mkono ajenda yetu ya kuendeleza uchumi wa kidijitali,” alisema Silas.

Kampeni ya Tap Tap Utoboe ilikuwa sehemu ya jitihada za Benki ya Exim kuhimiza jamii kufanya miamala kwa njia za kielectroniki, ikiwemo kupitia simu za mkononi na mtandao, sambamba na malengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya kuimarisha matumizi ya mfumo wa kifedha wa kidijitali.

About The Author

error: Content is protected !!