KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amedai kuwa vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji ya raia nchini unakihujumu chama chake na kukigombanisha na wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
“Tunasema bila mashaka kwamba watu wenye nia mbaya ndio wenye kuendesha magenge ya uhalifu katika nchi yetu, kwa nia ya kukikosanisha chama chetu na wananchi, pamoja na kutaka kuparanganisha taifa letu,” ameeleza.
Balozi Dk. Nchimbi ameeleza hayo leo, tarehe 13 Septemba 2024, jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na waandishi wa habari wandamizi nchini, Ofisi Ndogo za chama hicho, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Alisema, “Mtu yeyote anayehatarisha usalama wa raia, mtu yeyote anayeshiriki katika kuteka raia, mtu yeyote anayeshiriki katika mauaji ya raia, ama kikundi chochote kinachofanya raia waishi kwa hofu, ni wazi kinajua kwamba kinafanya hivyo ili kuharibu taswira ya CCM mbele ya umma.”
Aliongeza: “Hakuna mtu ambaye anakitakia mema chama hiki na kukipenda, ataweza kuunga mkono matendo hayo ya utekaji, mauaji na utesaji.
“Na ndiyo maana, kama ni mtu ama ni genge la watu au mtu, linalojihusisha na utekaji nyara watu, linajihusisha na mauaji ya watu, haliwezi kuwa na nia njema na CCM.”
“Ni mwendawazimu peke yake anayeweza kutamka kwamba CCM inaweza kufanya jambo la kujiumiza yenyewe…CCM siyo chama cha watu wajinga, ni watu wanaojua kila unachofanya kina matokeo gani,” amefafanua.
Amesema, madhara ya vitendo vya utekaji na mauaji, ni umma kuikataa CCM na kwamba chama chochote cha siasa hakiwezi kuratibu uhalifu huo.
“Ni chama cha siasa kisichojitambua ambacho kinaweza kusimamia, kuratibu au kufanya matendo yanayofanya kikosane na wananchi wake. Na ndio maana (CCM), tunapita kila siku kuelezea utekelezaji wa ilani. Tunafanya hivyo, ili kutafuta uungwaji mkono. Kwa hiyo, hatuwezi kufanya haya yanayotendeka,” ameeleza.
Amesema, katika kueleza utekelezaji huo, viongozi wa chama hicho pia wamekuwa wakiainisha maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
Amesema, utekelezaji wa ilani hiyo ya mwaka 2020-2025, umekamilika kwa asilimia 98 nchi nzima na kinachofanywa na CCM hivi sasa ni kuendelea kuwaomba wananchi wawe na imani nacho.
Hata hivyo, hata baada ya kuulizwa ni akina nani wanaohujumu serikali, Dk. Nchimbi hakutaja wanaogombanisha chama chake na wananchi; na au wanaogombanisha serikali na wananchi.
Badala yake, kiongozi huyo alisisitiza kuwa “wanaohujumu chama chetu au serikali yetu, wanaweza kuwa ndani ya CCM, ndani ya serikali au nje ya chama na serikali.”
Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kauli ya katibu mkuu wa CCM, yaweza kusaidia kupunguza hasira za wananchi dhidi ya vitendo vya utekaji, kwa kuwa wengi wao walikuwa wanadhani vitendo hivyo, vinabara na serikali au chama kilichoko madarakani.
ZINAZOFANANA
Morocco kuwapa wanawake haki zaidi
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Ushindi wa Profesa Lipumba wapingwa