December 27, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tanzania kutengeneza mkakati wa muda mrefu wa kaboni

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Ashatu Kijaji amesema Tanzania iko katika hatua za awali za kutengeneza mkakati wa muda mrefu wa kaboni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema hayo wakati alipokutana na mabalozi wanaoziwakilisha nchi nne nchini ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa nyakati tofauti leo Septemba 12, 2024.

Akizungumza na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasuhi Misawa, Dk. Kijaji amesema kuwa Serikali ina nia ya dhati katika kuelekea kwenye uchumi wa chini wa kaboni na kukuza mbinu za maendeleo endelevu.

Ameiomba Japan kushirikiana na Tanzania katika sema kuwa  na kwa sasa iko katika utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Kupika Safi 2024-20234 ambao gharama yake ni takriban Dola za Kimarekani bilioni 1.8 (zaidi ya Sh. 4.6 trilioni).

Pia, ameiomba Serikali ya nchi hiyo kuimarisha uwezo wa Kituo cha Kitaifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) na kuongeza uwezo wa kiufundi kwa ajili ya kufanya Tathmini ya Athari za Mabadiliko ya Tabianchi.

Akizungumza na Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud Al Shidhani, Waziri Dk. Kijaji amesema Tanzania imechukua hatua zote kuhakikisha inakabiliana na athari za kimazingira.

Aidha, ameomba ushirikiano na Oman katika utekelezaji wa uchumi wa bluu na miradi inayohusiana na mifumo ya tahadhari ya mapema na upangaji wa anga ya Baharini.

Hali kadhalika, katika urejeshaji wa mfumo ikolojia ikiwemo kusaidia kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa Ofisi ya Makamu wa Rais kuratibu masuala ya mabadiliko ya tabianchi katika sekta mbalimbali.

Ameiomba Oman kushiriki katika kuboreshaji wa programu za mfumo wa chakula wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi na kusaidia kuimarishaji wa uwezo wa Kitaasisi kufuatilia fedha za mazingira.

Katika hatua nyingine, Waziri Dk. Kijaji amefanya mazungumzo na Balozi wa Uturuki hapa nchini, Dk. Mehmet Gulluoglu pamoja na Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini Yahya Okeish kwa nyakati tofauti.

Katika mazungumzo hayo viongozi hao wamejadili kuhusu ushirikiano katika miradi ya nishati mbadala, mipango ya ufanisi wa nishati ikijumuisha teknolojia ya kupikia safi na mifumo endelevu ya usafirishaji.

Ameomba kuanzishwa kwa ushirikiano kwa ajili ya kujenga uwezo, kuhamisha teknolojia, na uwekezaji katika mradi wa nishati mbadala kama vile nishati ya upepo, jua na umeme wa maji na usimamizi na udhibiti wa viumbe vamizi katika nyanda za malisho, ardhi ya kilimo, maeneo ya hifadhi na maeneo ya wazi.

Vikao hivyo vimehudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais,Christine Mndeme na Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria Ofisi ya Makamu wa Rais Dustan Shimbo.

About The Author

error: Content is protected !!