BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imetoa wito kwa wafanyabaishara wa kitanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara baina ya Tanzania na Afrika kusini huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuchochea na kuwezesha biashara baina ya mataifa hayo mawili kupitia ukuzaji wa mitaji na urahisishaji wa miamala. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Wito huo umetolewa na Mkuu wa kwa Kitengo cha Wateja Wakubwa wa Kimataifa wa NBC, Bw Wilson Nkuzi wakati akizungumza kwenye Mkutano wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini nchini Tanzania (SABF) uliofanyika jijini Dar es Salaam jana jioni.
Mbali na wanachama ambao ni wafanyabiashara baina ya mataifa hayo mawili hapa nchini, mkutano huo pia ulihusisha wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali, maofisa wa ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania pamoja na maofisa kutoka benki ya NBC ambayo ndio ilikuwa mdhamini mkuu wa mkutano huo.
Kwa mujibu wa Nkuzi, kupitia huduma zake mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo ya ukuzaji mitaji, dhamana, huduma ya fedha za kigeni sambamba na huduma ya malipo kwa njia ya mtandao inayofahamika kama ‘NBC Connect’ benki hiyo imedhamiria kurahisisha zaidi ufanisi wa biashara kwa wafanyabiashara hao ili waweze kushiriki kwa ushindani zaidi kwenye fursa hiyo ya kimataifa.
“Kinachotupa msukumo zaidi katika jitihada hizi ni ongezeko kubwa la wafanyabiashara baina ya mataifa haya mawili ambao wamekuwa wakitumia fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na NBC mahususi kwao ikiwemo mikopo ya ukuzaji mitaji, dhamana, miamala ya kimataifa na zaidi huduma ya kubadilisha fedha za kigeni ambapo licha ya changamoto ya upatikanaji wa dola za Kimarekani nchini, NBC tunapambana kuhakikisha wafanyabaishara hawapitii changamoto hiyo,’’ alisema.
Zaidi Bw Nkuzi alielezea utayari wa benki hiyo kuunga mkono jitihada za serikali katika kufanikisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali hapa nchini kupitia utoaji wa dhamani za benki (Bank Guarantee) katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.
Kwa muda mrefu sasa benki hiyo imekuwa mdau mkubwa wa wafanyabiashara kati ya Afrika Kusini na Tanzania. Licha ya udhamini wake kwenye mkutano huo pia benki hiyo ni mwanachama kutokana na umiliki wa asilimia 55 wa kampuni ya ABSA Group ya nchini Afrika Kusini kwenye benki hiyo.
Mkuu wa Miamala na Amana za Wateja Wakubwa wa NBC, Jimmy Myalize alipata wasaa wa kuelezea huduma mbalimbali za benki hiyo mahususi kwa wadau hao sambamba na mchango wa benki hiyo katika kusaidia jamii hususani kupitia udhamini wake kwenye sekta mbalimbali mbali ikiwemo michezo na sekta ya afya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Manish Thakrar alisema pamoja na mambo mengine, nia ya jukwaa hilo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini Tanzania, huku akitaja suala la upatikanaji wa huduma za kifedha za uhakika kama moja nguzo muhimu katika kufanikisha agenda hiyo.
“Uwepo wa jukwaa hili umekuwa na tija kubwa sana miongoni mwetu kama wanachama kwa kuwa tumekuwa kukijadili fursa mbalimbali baina yetu kama wafanyabiashara, baina yetu na serikali zetu na fursa zinazotoka nje mataifa yetu.’’
‘’Hiyo ndio sababu leo tumejadili pia kuhusu mkutano unaondelea huko China baina ya China na mataifa ya Afrika ili kuona namna gani sisi kama wafanyabiashara tunaweza kuguswa na fursa zitokanazo na maazimio ya mkutano huo,’’ alisema Thakrar huku akiishukuru benki ya NBC kwa kuendelea kuwa mdau muhimu katika kufanikisha mikutano hiyo.
Kwa mujibu Thakrar biashara baina ya Tanzania na Afrika Kusini imeendelea kukua zaidi hususani kwenye mauzo ya bidhaa za viwandani, madini pamoja na mazao ya kilimo huku akitoa wito kwa wafanyabiashara wa kitanzania kuendelea kutumia vema uhusiano uliopo baina ya mataifa hayo mawili kufanikisha biashara mbalimbali ikiwemo mazao ya kilimo.
ZINAZOFANANA
Shindano la Mabingwa Expanse kukupa mamilioni Sikukuu hii
Cat Purry Kasino mtandaoni makulipo makubwa
Michuano ya Expanse kukupa mkwanja msimu huu wa Sikukuu