September 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Waziri Dk. Kijaji ahimiza usimamizi wa mazingira viwandani

 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Ashatu Kijaji amewataka wamiliki wa viwanda nchini kuweka mifumo ya majitaka kuepusha yasitiririke ovyo na kuchafua mazingira na kuathiri afya za wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Amesema Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla inatambua umuhimu wa wawekezaji hivyo inaendelea kuwaelimisha namna bora ya kufuata sheria ya mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa.

Dk. Kijaji amesema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika kiwanda cha kurejeleza taka za mifuko chakavu na za plastiki kwa ajili ya kuzalisha viatu, mabomba na mifuko cha Future Colorful kilichopo jijini Dodoma alipfanya ziara ya kukagua uzingatiaji wa sheria ya mazingira, tarehe 4 Septemba, 2024.

Amesema wenye viwanda wanapaswa kutafuta njia bora ya kuyarejeleza ili yatumike tena katika shughuli za viwanda, hatua itakayowapunguzia pia gharama ya matumizi ya maji hayo.

Katika ziara hiyo Dk. Kijaji alibaini shehena ya taka hizo ambazo zinatumika kama malighafi ikiwa imekusanywa bila kufunikwa hivyo alielekeza uongozi wa kiwanda hicho kuihifadhi vizuri kwa kuhakikisha inafunikwa.

“Tunawapongeza sana kwa kukusanya taka hizi na kuzirejeleza lakini changamoto tuliyoiona hapa ni hizi taka kuwa wazi hivyo, ni muhimu kuandaa mazingira mazuri ya kuzihifadhi, mvua ikinyesha zinakuwa taka na sio malighafi tena ipigwe sakafu mfuniko wa kufunika malighafi hizi,“ alisisitiza Dk. Kijaji.

Aidha, Dk. Kijaji amewataka wawekezaji wa viwanda kuwaajiri wataalamu wa mazingira watakaofanya kazi nao kuhakikisha masuala muhimu na maelekezo kuhusu utunzaji wa mazingira yanafuatwa.

Pamoja na hayo ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa na vifaa vya vyaa ili kuwakinga kutokana na kugusa au kunusa taka zinazokusanywa ili kulinda afya zao.

Katika hatua nyingine ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuwapatia nambari ya malipo ili waweze kutekeleza wajibu wao wa kulipa faini wanayotakiwa kutokana na kukiuka kanuni ya katazo la mifuko ya plastiki kipindi kilichopita.

Hata hivyo, Dk. Kijaji amewapongeza kwa kurekebisha dosari hiyo na kuanza kuzalisha mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira aina ya ‘non-woven’.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Wang Dajing kupitia kwa msimamizi wa kiwanda Zakia Juma ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na Serikali.

Amemuomba Dk. Kijaji na Ofisi yake kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji hapa nchini kwa kupatia elimu kuhusu katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Katika ziara hiyo Waziri aliambatana na Afisa Mazingira Mhandisi Joseph Kiruki, Meneja wa NEMC Kanda ya Kati Dk. Caren Kahangwa na Afisa Mazingira wa NEMC, Innocent Makomba.

About The Author