September 20, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi 5 wanaodaiwa kumtorosha mfungwa aliyeua wanawake 42, waburuzwa mahakamani

 

MAOFISA watano wa polisi wanaotuhumiwa kumsaidia mfungwa anayehusishwa na mauaji ya wanawake 42 kutoroka gerezani jijini Nairobi, wamefikishwa mahakamani. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).

Hatua hiyo inajiri wakati huu wakati oparesheni kali ikiwa imeanzishwa kumsaka Collins Jumaisi, mshukiwa wa mauaji ya wanawake hao aliyetoroka mahabusu pamoja na raia wengine 12 Eritrea.

Jumaisi (33), alikamatwa na polisi mwezi uliopita baada ya kupatikana kwa miili ya wanawake waliouawa ikiwa imetupwa kwenye eneo la kutupa taka jijini Nairobi.

Inadaiwa kwamba wafungwa hao walitoroka gerezani kwa kukata sehemu ya paa kwenye gereza walimokuwa wanazuiliwa.

Kwa mujibu wa Kaimu Inspekta Jenerali wa polisi nchimni Kenya, Gilbert Masengeli, wafungwa hao walisaidiwa kutoroka.

Maofisa watano kati ya wanane waliokamatwa kwa kuhusishwa na njama hiyo wamefikishwa mahakamani leo Jumatano huku polisi wakitaka kuwazuia kwa siku 14 zaidi kumaliza uchunguzi wao.

Raia 12 wa Eritrea waliotoroka gerezani, walikuwa wamekamatwa kwa kuwa nchini Kenya kinyume na sheria.

Wafungwa wengine watano ambao hawakutoroka wakati wa tukio hilo, pia wanachunguzwa kwa mujibu wa taarifa ya maofisa wa polisi.

Kituo husika kipo katika mtaa wa kifahari wa Gigiri, mtaa ambao pia una makao makuu ya Umoja wa Mataifa pamoja na balozi zingine.

Idara ya polisi nchini kenya imesema Jumaisi alikamatwa tarehe 15 ya mwezi Julai baada kukubali kuwaua wanawake 42 katika kipindi cha miaka miwili tangu mwaka wa 2022, mke wake akiwa mwathirwa wa kwanza.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miezi sita, mfungwa anayekabiliwa na kesi kubwa kutoroka gerezani nchini Kenya.

Raia wa Kenya, Kevin Kangethe, anayekabiliwa na mashtaka ya kumuua mpenziwe nchini Marekani mwaka uliopita, Februari mwaka huu pia alitoroka gerezani.

About The Author