BARAZA la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) limeunda Kamati Maalum ya kufuatilia mgogoro wa baina ya wakazi asilia (wamasai) katika wilaya ya Ngorongoro na mamlaka za Serikali ili kupatikane suluhu ya kuduma ya migogoro kwenye eneo hilo. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi amesema kuwa kamati hiyo itafutilia mgogoro huo kwa kufika kwenye vijiji vya wilaya ya Ngorongoro.
Mwabukusi amesema kamati hiyo yenye mawakili wabobezi watano itakayoongozwa na Dk. Rugemeleza Nshala, Tike Mwambikile, Bumi Mwaisaka, Leticia Mtagazwa na Paul Kisibo.
Mwabukusi amesema kamati hiyo itakayofanya kazi kwa siku 30 kuanzia kesho tarehe 21 Agosti, itafanya mashauriano na taasisi mbalimbali na kutembelea eneo lenye migogoro ili kujua uhalisia wa migororo.
“Kamati itafanya mapitio ya sera, sheria, mazoea pamoja na kuzichambua kuhusiana na umiliki kwa wazawa pamoja na shughuli za uwekezaji, uhifadhi na kubaini uzingatiaji wa haki za msingi za raia katika maeneo husika,” amesema.
Amesema kamati hiyo itaandaa kongamano maalum la kitaifa kuhusiana na namna bora ya kufanya maendeleo kwa kuzingatia na kulinda haki za wazawa katika ardhi zao za asili pamoja na haki zao za kijamii, kiuchumi, kiutamaduni katika maeneo yanayofikiwa na shughuli za uwekezaji.
Amesema kuwa kamati hiyo itafuatilia mienendo mbalimbali ya kesi zinazotokana na migogoro mbalimbali ya ardhi nchini.
“Kamati itafanya kazi ya kubainia mashauri au hatua zote ambazo zimechukuliwa na walalamikaji pamoja na walalamikiwa kisheria na kiutaratibu katika kuzingatia sheria na kubaini majina ya watu ambao kweli wameridhia kuondoka kwa hiyari yao na ambao hawajakubali kuondoka kwa sababu ya wao kuamua kubaki katika maeneo yao ya asili la Ngorongoro,” amesema Mwabukusi
Amesema kamati italishauri baraza la uongozi la TLS hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa kudumu juu ya migogoro ya ardhi inayosababishwa uwekezaji na uhifadhi.
Mwabukusi amesema kamati hiyo itaisaidia TLS kutekeleza wajibu wake wa kisheria wa kuishauri Serikali na kulinda haki za wananchi ili kupata suluhisho la kudumu.
Aidha, katika hatua nyingine Mwabukusu ameeleza kushangazwa na hatua ya Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa kufuta vijiji kadhaa wilaya ya Ngorongoro na kufafanua kuwa hatua hiyo ya waziri ni kinyume cha sharia kwani hana mamlaka kufuta vijiji hivyo.
ZINAZOFANANA
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu