September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Samia afungua skuli iliyojengwa na NMB kwa mil. 800

 

RAIS Samia Suluhu Hassan amefungua Skuli ya Maandalizi ya Tasani – Visiwani Zanzibar ambayo Benki ya NMB imegharamia ujenzi wake na uwekaji wa samani ikiwemo viti, meza na madawati kwa gharama ya Sh 800 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Skuli hiyo yenye madarasa matano na itaweza kupokea wanafunzi 200 kwa wakati mmoja.

Akizungumza katika ufunguzi wa shule hiyo leo Jumanne, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alimueleza Rais kuwa ujenzi wa shule hiyo ni muendelezo wa mchango wa Benki ya NMB katika kuchangia ukuaji wa elimu nchini.

Amesema kwa kutambua mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuinua sekta ya elimu nchini, shule hiyo imepewa jina la Dk. Samia Suluhu Hassan.

Pamoja na mambo mengine amesema skuli hiyo pia imejumuisha ofisi za walimu, sehemu ya michezo ya watoto na miundombinu mingine.

“Tukiwa wadau wa karibu wa maendeleo nchini, tunaamini skuli hii itahudumia vizazi ambavyo kwa baadae vitakuja kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Zaipuna.

About The Author