SAKATA la binti anayedaiwa kubakwa na kulawitiwa na vijana watano, limechukua sura mpya baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini – IGP, Camilius Wambura kumhamisha Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, SACP Theopista Malya kwenda makao makuu ya polisi Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Malya ambaye nafasi yake imechukuliwa na SACP George Katabazi, amekumbwa na kadhia hiyo baada ya kudai kuwa binti huyo ambaye ni mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam, ni kama alikuwa anajiuza.
Licha ya video za ukatili huo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha vijana hao walitumwa na mtu anayeitwa Afande, Malya aliyezungumza na chombo kimoja cha habari, amenukuliwa akidai kuwa vijana hao wanne kati ya sita waliokamatwa, hawakutumwa na afande kwani walikuwa kama walevi na wavuta bangi.
Kutokana na mjadala mkali ulioendelea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu majibu ya aliyekuwa RPC huyo wa Dodoma, Jeshi la polisi kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na Msemaji wa Polisi, David Misime limeomba radhi kwa kila mmoja aliyechukizwa na kuguswa na majibu hayo ya SACP Malya.
“Jeshi la polisi lingependa kutoa taarifa kuwa kauli hiyo kama inavyoonekana kwenye hicho kichwa cha habari (RPC: Anayedaiwa kubaka na kulawiti kama anajiuza” siyo msimamo wa jeshi la polisi. Kauli sahihi ni kama zilivyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi kwa ummma tarehe 4,6 na 9 Agosti mwaka huu,” amesema Misime.
Pamoja na mambo mengine, taarifa hiyo ya Misime imeeleza kuwa watuhumiwa hao watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani leo tarehe 19 Agosti 2024.
Watuhumiwa hao waliokamatwa kwa kosa la kulawiti na kumbaka binti huyo ni Clinton Damask wa jina maarufu Nyundo, Praygod Mushi, Amini Lema na Nikson Jakson.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe