September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wakili Chuwa awasilisha maombi ya clip ya video kuletwa mahakamani

 

WAKILI wa Utetezi Edward Chuwa anayewatetea walalamikiwa Bhartat Nathwan na Sangita Bharat wanaotuhumiwa katika kesi ya kujeruhi na kutoa lugha chafu ya matusi, amewasilisha maombii mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea kwa hatua ya ushahidi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Chuwa aliomba Kiran Ratilal awasilishe kipande kifupi cha video (clip) kinachoonesha alivyotumbukizwa kwenye ndoo ya mchanganyiko wa saruji.

Hata hivyo, katika hatua za kisheria, wakili wa upande wa utetezi, alimuomba ushahidi shahidi huyo kuonesha kipande cha picha mjongeo (video/clip), inayoonesha tukio la kupigwa na kutumbukizwa katika ndoo yenye saruji.

Alitaka clip ili kujiridhisha na mazingira halisi ya tukio zima na eneo, jambo ambalo mlalamikaji hakuwa na ushahidi huo kwa wakati huo.

Katika usikilizaji wa kesi hiyo, ilielezwa mahakamani hapo kuwa eneo linalodaiwa kufanyika kwa tukio hilo kuna zaidi ya wakazi 40, lakini cha kushangaza hakuna hata mtu mmoja aliyejitokeza kuamulia ugomvi unaotajwa kutokea siku hiyo, jambo ambalo wakili wa upande wa utetezi alionesha mashaka.

Hata hivyo, ilielezwa kuwa aliyekuja kuamualia unaoitwa ugomvi, ni msimamizi wa jengo la makazi hayo, ambaye siyo mkazi wa eneo hilo, jambo ambalo pia lilizua viulizo vingi.

Uendeshwaji wa kesi hiyo, umechukua sura mpya baada ya kubadilishwa kwa wakili wa Serikali wa utetezi wa upande wa mashtaka, Wakili Grace Mwanga na kuletwa wakili mwingine kutoka Dodoma, Wakili Faraji Nguka kuendelea na uendeshwaji wa kesi hiyo.

Walalamikiwaji wa kesi hiyo ni wanandoa wawili Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wakituhumiwa kutenda makosa ya kujeruhi na kutoa lugha chafu dhidi ya mlalamikaji anayetajwa kwa majina ya Kiran Ratilal, tukio linalotajwa kutokea katika mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, Dar es Salaam, ikitajwa makosa hayo kutendeka mnamo Julai 21, 2023.

Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa kwa mara nyingine tena mnamo Agosti 30, mwaka 2024, saa tatu asubuhi, ambapo mashahidi wengine kwa upande wa mashtaka kusikilizwa zaidi, katika Mahakama ya Hakimu-Mkazi, Kisutu jijini Dar es Salaam.

About The Author