WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amezindua zoezi la uvuvi katika Ziwa Tanganyika baada ya kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo kwa miezi mitatu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kigoma … (endelea).
Waziri Ulega amezindua zoezi hilo katika Mwalo wa Katonga, Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma jana tarehe 15 Agosti 2024 na kubainisha kuwa kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu kulilenga kulinda na kuhuisha raslimali za uvuvi kwenye ziwa hilo.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Ulega mesema Serikali inatumia gharama kubwa kuzuia uvuvi haramu na kwamba Serikali itawachukulia hatua wavuvi wote watakaokuwa wanaojihusisha na uvuvi haramu.
“Serikali inafanya yote haya na kusitisha shughuli za uvuvi kwa muda si kuwakomoa wananchi wake kwani tunafuata mchakato wote kutoka kwa wataalamu wetu waliofanya utafiti na hatukurupuki kufanya maamuzi,” amesema Ulega.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amepiga marufuku watu watakaojihusisha na ulanguzi wa mazao ya uvuvi katika ziwa hilo na kutaka watu wanunue kwa bei za kawaida zinazojulikana kila siku.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Edwin Mhede amesema ni muhimu kulinda rasilimali za uvuvi kwa kuwa asilimia 10 ya Watanzania wapo kwenye sekta hiyo.
Amesema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2024 iliyofanyika ukanda wa Ziwa Tanganyika inaonyesha kuwa kuna wavuvi wapatao 32,757 ukilinganisha wavuvi 29,571 waliokuwepo kwenye matokeo ya sensa ya wavuvi waliokuwepo mwaka 2022.
Kuhusu mazao ya uvuvi, Mhede amesema mwaka 2023 zilipatikana tani 479,000 za samaki kwa nchi nzima sawa na Sh3.4 trioni na kati ya hizo tani 85 sawa na asilimia 17 zenye thamani ya Sh613 bilioni zilitoka katika Ziwa Tanganyika.
Baadhi ya wavuvi wa mwalo wa Katonga, wamesema kufunguliwa kwa ziwa hilo wanategemea kupata samaki na dagaa za kutosha na kwamba watatoa ushirikiano kwa Serikali dhidi ya uvuvi haramu.
Kido Jamal amesema walikuwa wanasubiria kwa hamu kuingia ziwani na kupata samaki kwani wameteseka kwa muda mrefu bila kula mgebuka wala dagaa.
Kwenye kikao kilichofanyika mwaka 2022 kikihusisha nchi zinazozunguka ziwa hilo – Zambia, Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uamuzi huo ni utekelezaji wa mkataba wa kikanda wa nchi wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika unaoweka hatua na taratibu za usimamizi endelevu wa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo.
ZINAZOFANANA
TRA yazindua ofisi ya walipa kodi binafsi
Mwenge wa uhuru wazindua mradi wa maji Kahangara -Magu
DC: Ilala hali ni shwari uandikishaji