September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

EACOP kuziinua kiuchumi kaya zilizoguswa na mradi bomba la mafuta

 

MRADI wa bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) umeanzisha programu ya kuzisaidia kaya ambazo ardhi yao limepita bomba la mradi huu. Lengo la programu hii ni kuziwezesha kaya kujiendeleza kiuchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Meneja wa Kitengo cha Ardhi na Ushirikishwaji wa jamii cha EACOP (Tanzania), Jean Lennock amesema kuwa lengo la mpango huu wa kuzisaidia kaya hizo ni kuondoa changamoto ambazo kaya hizo inakumbana nazo baada ya mradi kuzihamisha kaya hizo kutoka kwenye ardhi yao.

Nia ya mpango huu kuziwezesha kaya hizi kupata ujuzi na maarifa ya kuchangamkia fursa za biashara na kukuza biashara za kaya hizo katika maeneo yao.

Amesema kuwa katika kufanikisha shabaha hii, EACOP imeandaa programu 8 ambazo zitazisaidia kaya hizo kurejea katika maisha yao ya awali.

Ndani ya programu hizo, shughuli nane za kurejesha maisha ya kaya hizo zimebainishwa katika maeneo yaliyoathiriwa na mradi.

Shughuli hizi ni pamoja na kupewa elimu ya upandaji na upandikizaji wa mazao ya kilimo kama vile mahindi, ufugaji wa kuku, programu ya ufugaji bora wa wanyama, maboresho ya ufugaji wa nyuki, maendeleo ya biashara na mafunzo ya bajeti ya kaya na usimamizi wa fedha.

Amesema kuwa EACOP hivi karibuni imezindua utekelezaji wa program ya Maendeleo ya biashara.

Awamu ya majaribio kwa programu ya maendeleo ya biashara itakuwa katika Mkoa wa Kagera (hususani Wilaya za Misenyi na Muleba).

Awamu hii ya majaribio inalenga kaya 798 zilizoathiriwa (64 zikiwa zile ambazo zimeathiriwa maeneo yao kwaajili ya ujenzi wa Kambi na vituo vya kutunzia mabombana 734 ni zile ambazo zimeathiriwa ardhi yao kwenye mkuza wa bomba la mafuta).

Lennock amesema lengo kuu ni kuzisaidia na kuzijengea uwezo kaya 8,971 katika eneo la maendeleo ya biashara. Lengo hili pia linalenga maeneo 453 ya kipaumbele ya kaya 8,518 zilizo kando ya mkuza wa bomba la mafuta katika mikoa minane nchini Tanzania ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara naTanga.

Programu hii imebeba shabaha nyingine kubwa ambayo ni kufanya tathimini kamili ya uwezo na mahitaji ya kaya zilizoathiriwa, kushughulikia changamoto zilizozuia kaya hizo kusonga mbele kibiashara katika maeneo yao ya awali kabla hayajachukuliwa na mradi.

Amebainisha kuwa lengo ni kuziwezesha kaya zilizoathiriwa kusimamia mikakati yao ya maisha katika maeneo kama biashara ilikuwa na ukuaji endelevu wa kiuchumi.

Utekelezaji wa mpango huu ni kuhakikisha manufaa na thamani ya shughuli kubwa za maisha ya kila siku ya kaya husika zinakuwa endelevu.

EACOP Ltd. ni kampuni yenye madhumuni maalum, inayosimamiwa na Mkataba wa Wanahisa wake ambapo wanahisa ni TotalEnergies (62%), Uganda National Oil Company (UNOC – 15%), Shirika la Maendeleo ya Mafuta ya Petroli la Tanzania (TPDC – 15%) na CNOOC (8%).

About The Author