WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umesajili zaidi ya watoto milioni 10 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara, idadi ambayo ni sawa na asilimia 68 ya watoto waliopewa vyeti vya kuzaliwa ikilinganishwa na asilimia 13 wakati wanaanzisha mpango huo mwaka 2012. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu Barani Afrika yaliyofanyika wakati wa Sikukuu ya Wakulima katika viwanja vya Nanenane jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Dk. Khatibu Kazungu amesema hatua hiyo ni ya kupongezwa.
Amesema RITA wamefanya kazi nzuri ikiwemo utoaji bure wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano Tanzania bara.
Amesema serikali kupitia RITA imeanza kuchukua hatua madhubuti ya kuongeza kasi ya usajili kupitia mkakati wa kitaifa wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu.
“Kila ifikapo tarehe 10 Agosti kila mwaka, Tanzania inaungana na mataifa mengine Barani Afrika kuadhimisha siku hii muhimu iliyobeba kauli mbiu isemayo ‘Kuimarisha uhusiano wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu na mifumo ya kisheria ya utambuzi kwa njia ya kidijitali iliyo jumuishi,” alieleza, Dk. Kazungu
Aidha, Dk. Kazungu alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wataendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha mpango wa kuwasajili na kuwapatia vyeti vya kuzaliwa watoto wa umri chini ya miaka mitano unakuwa endelevu kwa kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anapata fursa ya kusajiliwa ndani ya muda mfupi na taarifa zao zinatumwa kwenda kwenye kanzidata ya RITA kwa wakati stahiki.
“Nitoe rai kwa wazazi kuhakikisha wanatumia fursa hii iliyotolewa na serikali ili kuwapatia watoto wao vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni nyaraka ya msingi ya utambulisho.” alisisitiza Dk. Kazungu
Dk. Kazungu alisema Usajili wa matukio yote muhimu ikiwemo vizazi, na vifo unaiwezesha serikali kupata takwimu sahihi kwa ajili ya kupanga mipango endelevu ya maendeleo kwa maslahi mapana ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi alisema maadhimisho hayo ya Nane Nane ambayo kitaifa huadhimishwa jijini Dodoma, yamelenga kujenga ufahamu kwa wananchi juu ya kumbukumbu muhimu pamoja na matukio muhimu ya vizazi, vifo, talaka, ndoa pamoja na kuasili watoto.
“Katika kuadhimisha siku hii, kuna shughuli mbalimbali ambazo tunazifanya, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma, kutoa huduma za usajili sambamba na kutembelea vituo vinavyofanya usajili wa matukio muhimu ya binadamu ili kubaini changamoto na kuzitafutia ufumbuzi,” alisema Kanyusi.
Kwa upande wake, Afisa Hifadhi wa Watoto kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Asnath Barnabas, mbali ya kuipongeza serikali kwa jitihada inazochukua katika kuhakikisha wanawafikia watoto wote chini ya umri wa miaka mitano katika mikoa yote Tanzania bara na kutoa vyeti bure, alisema UNICEF wataendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.
“Tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kuhakikisha watoto wote wanasajiliwa na kupewa vyeti sambamba na kuchukua kumbukumbu ya matukio yote muhimu ikiwemo vizazi, na vifo,” alisema Barnabas.
ZINAZOFANANA
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu