September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

GGML waanza kutumia umeme wa gridi, kupunguza gharama kwa 92%

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amezindua kituo cha kupokea na kupoza umeme katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (Geita Gold Mining Limited- GGML) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 34 na kuiwezesha GGML kuanza kutumia umeme wa gridi kwa matumizi yake badala ya mafuta na kupunguza gharama za uendeshaji kwa asilimia 92. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana Jumanne wilayani Geita mkoani Geita, Dk. Biteko amesema ujenzi wa kituo hicho ni alama halisi ya umoja na ushirikiano uliopo kati ya Serikali na sekta binafsi.

Amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa laini ya umeme ya KV 33 ambayo imejengwa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) kwa gharama ya Sh 8.04 bilioni huku GGML ikijenga kituo cha kupoza umeme kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 24.

Amesema GGML ilikuwa inatumia Sh 130 bilioni kwa mwezi kama gharama za uendeshaji na kwenye umeme wa mafuta ilikuwa inatumia Sh 13.4 bilioni kila mwezi na kuathiri mapato yake kwa Serikali, hivyo kuanza kazi kwa kituo hicho kunapunguza gharama za uendeshaji kwa mgodi na kupelekea Serikali kuongeza mapato yake, kuongeza ajira na pia GGML kutanua shughuli zake.

Dk. Biteko ameipongeza kampuni hiyo kwa kuanza kutumia umeme wa gridi ambao unapunguza gharama za uendeshaji ambapo ametoa angalizo kuwa, kupungua kwa gharama hizo kuguse pia watumishi kwa kuboresha maslahi yao.

Ameeleza umeme mwingi unaozalishwa kwa sasa unatoa uhakika wa kwenda kwa wananchi na walaji wakubwa kama GGML na kuweka mkazo kuwa, hayo ni matokeo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuijali sekta binafsi.

Vilevile, ameipongeza GGML kwa kuzipa kipaumbele kampuni za kizawa katika kutoa huduma kwenye mgodi huo na kusisitiza kuwa huo ndio msimamo wa Serikali ya Tanzania wa kuhakikisha kampuni za ndani zinapewa kipaumbele kwenye miradi mbalimbali.

Pia Dk. Biteko amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati, TANESCO na Taasisi nyingine za Serikali kujali sekta binafsi kutokana na manufaa yake ikiwemo kuwa walipakodi wakubwa na kuongeza ajira nchini.
Makamu Rais wa AngloGold Ashanti – GGML anayeshughulikia miradi endelevu na masuala ya ubia na ushirika Afrika, Simon Shayo ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na miundombinu madhubuti ya umeme inayowawezesha kufanya biashara kwa ufanisi.

Amesema mradi huo ni muhimu kwa GGML kwani unawawezesha kupata umeme wa gridi na kupunguza matumizi ya umeme wa mafuta ambapo gharama zitapungua kwa asilimia 92.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema hali ya umeme nchini kwa ujumla ni nzuri huku uzalishaji ukikidhi mahitaji na ziada kidogo.

Kuhusu usambazaji umeme mkoani Geita amesema kuwa Mkoa una vijiji 486 na kati ya hivyo vijiji 483 vina umeme sawa na asilimia 99.38.

Ameongeza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vitongojini mkoani Geita inaendelea ambapo kati ya vitongoji 2,197, vitongoji takriban 1000 tayari vina umeme.

Ameongeza mkoa wa Geita umetengewa Sh 8.5 bilioni kwa ajili ya kupeleka umeme maeneo ya migodi na viwanda na utekelezaji umefikia asilimia 41.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amemshukuru Rais Samia kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ambayo yamepelekea wawekezaji kufanya kazi na kuletea nchi faida akitolea mfano kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu GGM imezalisha tani 51 za dhahabu ambayo ni mafanikio makubwa yanayochangia ukuaji wa pato la Taifa.

Amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha umeme kufika pia kwenye migodi ya wachimbaji wadogo ambapo katika kipindi cha miaka mitatu wachimbaji wadogo 19 wamepelekewa umeme kwenye migodi yao na kuwezesha uzalishaji wa kilo za dhahabu takriban 11,000.

Wabunge mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Rais Samia pamoja na uongozi wa wizara ya nishati kwa kutekeleza mradi huo ambao una umuhimu mkubwa kwa uchumi wa nchi na mgodi wenyewe.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Abubakari Issa amesema kuzinduliwa kwa kituo hicho kutaiwezesha GGML kuanza kutumia umeme wa gridi kwenye matumizi yake pamoja na kuongeza mapato ya TANESCO ambapo inategemewa yataongezeka kwa kiasi cha shilingi bilioni 2 hadi 3 kwa mwezi.

About The Author