October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TCB: Tuna imani na uzoefu mkubwa wa Lilian Mtali

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Tanzania (TCB), Adam Mihayo amesema ana imani na uzoefu mkubwa wa Lilian Mtali ambaye ameteuliwa na benki hiyo kuwa Mkurugenzi wa Biashara za wateja Wadogo na wa Kati. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumzia ujio wa Mtali katika Benki ya TCB, Mkurugenzi huyo amesema pia ana imani na uwezo wake wa uongozi hivyo ni matumaini ya benki hiyo kwamba atakuwa msaada mkubwa wakati huu wanapoendelea kuboresha huduma za wateja wa rejareja, wadogo na wa kati.

Amesema Mtali ana uzoefu wa miaka 26 katika sekta ya huduma ya kifedha akibobea katika usimamizi na uongozi wa huduma za biashara za wateja wateja wadogo, wa kati na wakubwa.

Taarifa hii imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma TCB imesema Mtali amefanya kazi na kupata uzoefu wa uongozi kutoka benki mbalimbali za hapa nchini na za kimataifa, amefanya kazi katika benki za I&M Bank Tanzania Limited, Standard Chartered, Stanbic na DCB akishika nyadhifa mbalimbali za uongozi kama Meneja wa tawi, Mshauri wa Masuala ya Fedha, Meneja Uhusiano wa Wateja, Meneja wa Huduma kwa Wateja na Ubora wa Huduma na Mkuu wa Kitengo cha Biashara kwa Wateja Wadogo na Wakubwa.

Kuhusu utendaji wake, amesema Mtali amefanya mabadiliko makubwa katika ukuaji na maendeleo ya taasisi zote alizofanya kazi. Amesimamia miradi mbalimbali ya kibenki kwa ujumla ikiwemo kuongeza wigo wa mikopo ya biashara kwa wateja wadogo, kusimamia ukuaji wa wateja binafsi, kusimamia ukuaji wa huduma za uwakala usimamizi, na mikopo ya kidigitali.

Mtali anatajwa kuwa nguzo ya uongozi, katika kuleta mabadiliko chanya ya taasisi na kuchochea mabadiliko ya uendeshaji biashara na utendaji wa taasisi.

Historia yake kitaaluma inaonesha Mtali ana Shahada ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Kimataifa cha Amerika (IUA), London Campus, United Kingdom na Cheti kutoka Modern Tutorial College, London, United Kingdom.

Pia amesoma kozi na semina mbalimbali za uongozi wa kimataifa kutoka United Kingdom, Afrika Kusini, Kenya, Zimbabwe, Angola na Singapore.

About The Author