RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi amelaani kitendo cha udhalilishaji na ukatili wa kijinsia aliofanyiwa binti mmoja mkazi wa Yombo Dovya huku akirekodiwa video na wanaume waliokuwa wakimtendea uovu huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Pia amesema TLS inalitaka Jeshi la Polisi kuchukua hatua stahiki za kisheria pamoja na kuhakikisha wahalifu wote waliotenda kitendo hicho na waliowezesha kutendwa kwa kitendo kile kiovu wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani mara moja ili haki iweze kutendeka.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu na TLS na kusainiwa Mwabukusi, imesema tukio hilo sio tu ni kinyume na sheria za nchi yetu lakini pia ni kinyume na maadili na utamaduni wetu kama Watanzania.
Aidha, amesem TLS inapinga vitendo vyote vya kikatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na iko tayari kushirikiana na vyombo vyote vya usalama na haki jinai katika kuhakikisha wahalifu hao wanafikishwa katika mamlaka sahihi za haki ili kujibu mashitaka yao.
“TLS pia kupitia kifungu cha 4 (e) cha Sheria iliyounda TLS (Tanganyika Law Society Act, Cap. 307 R.E. 2002) inaendelea kufuatilia mwenendo wa suala hili kwa ukaribu zaidi kwa kushirikiana na vyombo vya usalama na vinavyosimamia haki jinai ili kuhakikisha hatua stahiki kwa waliohusika zinachukuliwa kwa wakati na kwa mujibu wa Sheria.
“Kila binadamu anastahili heshima, haki na usawa katika jamii yetu. TLS inatoa wito kwa jamii kusimama pamoja kupinga udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia wa aina yoyote ile ikiwemo kuacha mara moja kusambaza video zinazohusu tukio hili ili kulinda haki ya mhanga.
Tanzania bila udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili wa kijinsia inawezekana,” amesema Mwabukusi.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe