December 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yaahidi kunogesha ushindani zaidi Ligi Kuu Bara

 

Mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC, Benki ya NBC jana Alhamisi ilishiriki kikamilifu kwenye tukio la utoaji wa tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini, TFF 2023/2024 huku ikiahidi kuendelea kushirikiana na wadau wote wa ligi  tatu inazozidhamini ikiwemo Ligi Kuu ya NBC, NBC Championship na Ligi ya Vijana ya NBC ili kuvijengea uwezo utakaochochea ushindani zaidi miongoni mwao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya NBC, Waziri Barnabas aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Theobald Sabi alisema benki hiyo imejipanga zaidi kuhakikisha kwamba udhamini wake kwenye ligi hizo unakuwa chachu muhimu katika kuvisaidia vilabu hivyo kuwa bora zaidi kupitia usajili wa wachezaji wenye viwango vizuri zaidi sambamba na kuboresha mabenchi yao ya ufundi.

“Leo hii kila mtu ni shahidi wa namna ambavyo tuzo hizi zimeongeza mvuto mbele ya wapenda soka wote hapa nchini kutokana na ushindani mkubwa uliopo miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwania tuzi hizi wakiwemo kutoka ndani na nje ya nchi

“Ushindani huu unatokana na ubora walionao wachezaji husika ambao chimbuko lake ni usajili mzuri unaofanywa na vilabu vinavyoshiriki ligi hizi. Jukumu letu kama wadhamini wakuu wa ligi hizi ni kuhakikisha kwamba vilabu vinaendelea kuwa na nguvu hiyo zaidi,’’ alibainisha Waziri.

Katika tuzo hizo ilishuhudiwa maofisa mbalimbali wa benki hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya wateja wadogo na Wakubwa wa benki hiyo , Elibariki Masuke, Mkuu wa Kitengo cha Mikakati wa Benki  wa benki hiyo, Msafiri Shayo na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo, Raymond David wakikabidhi tuzo kwa washindi mbalimbali wa tuzo hizo.

Aidha Waziri akipata heshima ya kushiriki sambamba na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa   kukabidhi Tuzo ya Mchezaji Bora Ligi Kuu ya NBC  (MVP) kwa mchezaji Aziz Ki kutoka klabu ya Yanga SC ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia heshima hiyo ni kwa niaba ya maofisa wengine na Mkurugenzi Mkuu wa  benki hiyo, Theobald Sabi, Waziri  alisema imekuwa ni fahari kwao kama  wadhamini wakuu kupewa heshima hiyo hali iliyothibitisha thamani ya mrejesho chanya kutoka kwa wadau wa mchezo wa mpira hapa nchini.

“Heshima hii tunayoendelea kuipata kupitia mchezo huu pendwa inatusukuma zaidi kuendelea kuwekeza nguvu zetu zaidi si tu kwenye mchezo huu bali pia michezo mingine ikiwemo riadha, golf na michezo mingine ambayo imekuwa ikitusaidia kusukuma agenda zetu mbalimbali zinazolenga kusaidia jamii hususani kwenye masuala ya afya ya mama na mtoto.’’ Aliongeza.

About The Author

error: Content is protected !!