December 11, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TCB yazindua huduma inayowezesha wateja kulipia tiketi za usafiri SGR

 

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua huduma ya Popote Akaunti inayomuwezesha mteja kufungua akaunti na kupata huduma za kibenki kidijiti pamoja na kufanya malipo mbalimbali ikiwemo kulipia tiketi za Reli ya Kisasa (SGR). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ofisa Mkuu wa Huduma za Kidijiti na Ubunifu TCB, Jesse Jackson amebainisha hayo leo Jumanne alipozungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam.
Jesse alisema huduma hiyo itasaidia jamii hasa ambayo inaishi maeneo ya vijijini na iliyombali na huduma za kibenki.

Jesse amesema kubuniwa kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa dhamira thabiti ya Benki ya TCB katika kuwezesha ujumuishi wa kifedha na kutumia maendeleo ya teknolojia katika kuongeza upatikanaji wa huduma za kibenki.

“Uzinduzi huu wa akaunti ya TCB POPOTE ni mfano hai wa dhamira yetu ya kuelewa mahitaji ya wateja wetu na kuwaletea ubunifu unaochangia ukuaji uchumi wa taifa kwa kuzifanya huduma za kibenki kupatikana kwa watu wote” amesema Jesse.

Amesema kuwa benki hiyo itaendelea kubuni huduma ambazo zitasaidia kupeleka huduma za kifedha karibu na wateja nchini.

“Bado kuna uhitaji wa kusogeza huduma kwa wateja wetu na watanzania kwa ujumla, takwimu zinaonesha asilimia 89 ya watanzania wanaweza kupata huduma za kifedha ndani ya kilomita 5 na asilimia 22 tu ya watanzania wana akaunti za kibenki maana yake bado kuna uhitaji wa kusogeza huduma hizi za kifedha” amesema.

Awali Mkurugenzi wa Masoko na Ukuzaji Biashara na Mahusiano ya Umma, Deo Kwiyukwa alisema kuwa huduma hiyo inapatikana baada ya kufungua akaunti kwa gharama ya shilingi 1,000.

“Kwenye hii huduma mpya tumeongeza vionjo vingi anaweza kupata huduma zote za kibenki mfano kulipia bili mbalimbali na hivi karibuni tumezindua uuzaji wa tiketi kwa kishirikiana na Shirika la Reli (TRC) sasa huduma hii itamuwezesha huyo mteja mwenye akaunti kununua tiketi.

“Hiyo tiketi itakuwa na QR code haitaji kuiprinti ila anaweza kufanya hivyo ataionesha tu kwenye yale Magati ya kuingilia kwenye Treni ya Kisasa na kuingia moja kwa moja” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!