September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Majaliwa aipongeza NBC kwa kuboresha sekta ya Afya nchini

 

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepongeza jitihada za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) katika kuendeleza sekta ya afya hapa nchini kupitia huduma za kibenki pamoja program zake mbalimbali zinazolenga kuboresha sekta hiyo muhimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa pongezi hizo mapema leo Jumanne alipotembelea banda la maonyesho ya huduma za benki hiyo mahususi kwa wadau wa sekta ya afya lililopo kwenye kongamano la Afya Kitaifa lililoandaliwa na Taasisi ya Benjamin Mkapa (BMF) katika ukumbi wa JNICC dar es salaam.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa fupi kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Mahusino ya Umma wa benki ya NBC, Godwin Semunyu kuhusu jitihada mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo kwenye sekta afya, Majaliwa alisema serikali inathamini mchango mkubwa unaofanywa na benki hiyo pamoja na wadau wengine katika kusaidia sekta hiyo muhimu.

“Ni juzi tu nimetoka kuongoza mbio za NBC Dodoma Marathon zilizofanyika huko Dodoma ambapo jumla ya Sh 300 milioni zilikusanywa na NBC kwa ajili ya kusaidia jitihada mbalimbali za kiafya hususani kuokoa Maisha ya mama na mtoto.

“Huko Zanzibar pia wamekuwa wakifadhili huduma za uchunguzi wa bure kwa wanawake wajawazito kupitia huduma ya kliniki inayotembea pamoja na jitihada nyingine nyingi…hongereni sana NBC,” alipongeza.

Akiwa kwenye banda hilo pia Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliipongeza benki hiyo kwa jitihada hizo kwenye sekta ya afya huku akiahidi kuendelea kushirikiana na benki hiyo katika kutekeleza miradi mbalimbali kwenye sekta ya afya hususani ile inayolenga afya ya mama na mtoto.

Awali akizungumzia jitihada mbalimbali za benki hiyo kwenye sekta ya Afya, Semunyu alisema ikiwa kama mdau muhimu kwenye sekta hiyo, benki ya NBC mbali na kutoa huduma za kibenki kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo ikiwemo mikopo ya ujenzi wa majengo na miundombinu mbalimbali ya afya na ununuzi wa vifaa vya afya pia imekuwa ikifadhiri na kuendesha program mbalimbali za kiafya hapa nchini.

“Mbali na NBC Dodoma Marathon ambayo tumetoka kukusanya milioni 300 kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kina mama sambamba kufadhili masomo ya wakunga 100 kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa pamoja na ujenzi wa chumba cha upasuaji Hispitali ya Taifa Muhimbili pia tumekuwa tukishirikiana na makampuni ya bima katika utoaji wa bima ya afya,” alitaja.

Zaidi Semunyu alitaja jitihada nyingine za benki hiyo kwenye sekta ya afya kuwa ni pamoja na ufadhili wa mali za biashara ambapo benki hiyo inatoa mikopo bila dhamana kwa watoa huduma za afya pamoja na kutoa misaada ya vifaa vya matibabu kwa hospitali katika mikoa mbalimbali nchini.

About The Author