December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yakataa kusajili chama cha Gen Z

 

JARIBIO la watu kusajili vyama vya kisiasa nchini Kenya vyenye jina, Gen Z ili kuvuna wafuasi wa kisiasa kutokana kampeni zilizoanzishwa na vijana hao kupigania uongozi bora nchini zimezimwa na ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa nchini humo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).

Msajili wa vyama vya siasa nchini humo, Anne Nderitu amefichua kuwa tangu kuwepo kwa maandamano ya vijana hao wa kizazi cha sasa waliolenga kupinga Muswada wa Fedha wa 2024, Ofisi yake imepokea angalau maombi 20 kutoka kwa watu wanaotaka kusajili majina ya vyama vya kisiasa.

Hata hivyo, alisema maombi hayo yote, yanayoanza na maneno Gen Z, yamekataliwa kwani yanakiuka sheria, haswa kipengele 91 (1) (a) (e ) cha Katiba ya nchi hiyo kinachohusu masharti yanapaswa kuzingatiwa kuunda vyama vya kisiasa.

“Hitaji la sheria ni kwamba kila chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kiheshimu haki za watu kushiriki katika michakato ya kisiasa, yakiwemo makundi ya walio wachache na waliotengwa.

“Kwa hivyo, licha ya kupokea zaidi ya maombi 20 kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka tuhifadhi majina ya vyama vya kisiasa vinavyoanza na Gen Z, tumekataa maombi hayo kwa sababu yanakiuka Katiba,” alisema Nderitu.

Nderitu alisema ofisi yake ilianza kupokea maombi hayo baada ya siku ya kwanza ya maandamano hayo, tarehe 18 Juni 2024 kutoka kwa watu waliotaka kutumia umaarufu wa wimbi hilo umaarufu wa vijana kuvuna kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Watu hao walivutiwa na wimbi la vijana hao na hali kwamba hawakujinasibisha na kabila, kiongozi yeyote au chama chochote cha kisiasa.

“Chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kijumuishe watu wa umri na matabaka yote. Sharti tuone watu wa umri wote katika chama cha kisiasa. Ukisema chama cha Gen Z, unaonekana kuwatenga watu wengine,” alisema.

Chama kinachoonekana kuwatenga watu wa umri fulani, msajili huyo anasema, basi chama hicho kinakosa sura ya kitaifa.

About The Author

error: Content is protected !!