December 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Exim Bank yachangia vitanda kwa kituo cha Afya Tanga

 

BENKI ya Exim Tanzania imetoa jumla ya vitanda na magodoro 21 vya wagonjwa kwa kituo cha afya cha Mwakidila kilichopo jijini Tanga, mchango ambao umetatua kikamilifu tatizo la upungufu wa vitanda vya wagonjwa katika kituo hicho. Makabidhiano hayo, ambayo yamefanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mh. Balozi Dkt Batilda Burian, ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za afya katika mkoa huo. Kituo cha afya Mwakidila kilikuwa na vitanda 29 huku mahitaji yakiwa 50, hivyo mchango wa Exim Bank Tanzania umetatua tatizo hilo la muda mrefu katika hafla iliyofanyika mnamo tarehe 25 Julai 2024. Anaripoti Matilda Peter, Dar es Salaam … (endelea).

“Sekta ya afya nchini, ikiwemo mkoa wa Tanga, inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo uhaba wa vifaa vya matibabu, upungufu wa vitanda, madawa, pamoja na uchache wa watoa huduma za afya ambavyo vimekuwa vikiathiri kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma za afya,” anasema Bi Kauthar D’souza, Meneja Mkuu wa Idara ya Masoko na Mawasiliano, Exim Bank Tanzania.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo jijini Tanga, Bi D’souza aliongeza, “Sisi kama Exim Bank Tanzania, tunatambua changamoto hizi na ndo maana tunajitolea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya afya ili kusaidia Watanzania wapate huduma bora za afya.”

Takwimu zinaonesha jitihada za ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za Afya katika maeneo mbalimbali nchini ambao umewezesha vituo vya kutolea huduma za Afya kuongezeka kutoka vituo 8,549 Mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024; kama taifa tumepiga hatua katika kusogeza huduma hizi muhimu karibu zaidi kwa jamii.

Kwa muda sasa, Exim Bank imekuwa ikisaidia harakati mbalimbali za kuboresha huduma za afya katika maeneo mengine. Mwaka 2018, benki hiyo ilitoa vitanda vya wagonjwa kwenye hospitali katika mikoa 13, ukiwemo mkoa wa Tanga. Pia, mapema mwaka huu, Exim Bank iliendesha kampeni ya kitaifa ya uchangiaji damu katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha, na Mtwara.

Katika kuchochea matumizi ya kidijitali, hivi karibuni Exim Bank imezindua kampeni ijulikanayo kama ‘Tap Tap Utoboe’ ambayo imepata mafanikio kutokana na mwitikio mzuri wa wateja wa benki hiyo. Kampeni hii sio tu inahamasisha wateja kufanya miamala kwa njia ya mtandao na simu bali pia inaongeza matumizi ya kidijitali na kuunga mkono juhudi za Serikali katika dhamira yake ya kuelekea kwenye uchumi wa kidijitali.

Benki ya Exim Tanzania ni mojawapo ya taasisi kubwa na kongwe yenye matawi yake katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini Tanzania. Benki hiyo pia inajivunia kuwa benki ya kwanza ya Kitanzania kufungua tawi lake nje ya nchi ambapo mpaka sasa wanapatikana katika nchi za Djibouti, Comoro, na Uganda.

About The Author

error: Content is protected !!