Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Jumanne Muliro
WANAFUNZI watatu wa Shule ya Msingi Msongola iliyopo Kivule, wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, wamepoteza maisha baada ya kupigwa na radi wakiwa katika eneo la shule. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, aliyesema limetokea leo Jumatano 18 Machi 2026, wakati wanafunzi hao walipokuwa wakicheza.
“Ni kweli wanafunzi watano walikuwa wakicheza shuleni wakapigwa na radi, ambapo watatu walifariki papo hapo na wawili wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini,” amesema Muliro.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanafunzi wawili walionusurika wamekimbizwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi huku hali zao zikifuatiliwa na wahudumu wa afya.
Awali, Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kivule, Ojambi Massaburi, ilithibitisha tukio hilo na kutoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu pamoja na wote walioguswa na msiba huo.
“Mbunge anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo, akiwaombea faraja, uvumilivu na nguvu ya moyo katika wakati huu wa huzuni,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa jamii ya wakazi wa Kivule na wanafunzi kwa ujumla, huku mamlaka zikisisitiza tahadhari wakati wa mvua na radi.
ZINAZOFANANA
RITA yawapiga msasa wajumbe Bodi mpya ya wadhamini Kanisa la Waadventista Wasabato
CCBRT yarejesha furaha kwa wenye matatizo ya macho Dar
Jesca Magufuli: Uwezo wa kiongozi unapimwa kwa alama alizoacha