March 18, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

RITA yawapiga msasa wajumbe Bodi mpya ya wadhamini Kanisa la Waadventista Wasabato

 

KABIDHI Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi amewataka wajumbe wapya wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Waadventista Wasabato kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, kanuni na taratibu ili kuhakikisha mali za Kanisa hilo zinalindwa na kutumika kwa maslahi ya waumini wake. Anaripoti Mwandishi wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo, yaliyofanyika jana katika Ofisi za Makau Makuu ya RITA jijini Dar es Salaam. Kanyusi, amesema jukumu la Bodi hiyo ni kusimamia mali za kanisa hilo kwa niaba ya waumini hivyo wahakikishe wanatekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuepuka migogoro sambamba na kutimiza malengo ya kuanzishwa kwa kanisa hilo.

“Wadhamini wana wajibu wa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Bodi za Wadhamini Sura ya 318, hatutasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale watakaokiuka sheria, kwa kujimilikisha mali au kufanya ubadhirifu,” alisisitiza Kanyusi.

Amesema kuwa Bodi hiyo mpya itakuwa na wajumbe sita ambao ni David David Mpwani, Magulilo John Mwakalonge, Mathias Egid Mavanza, Shabatu Nicolaus Msaki, Joseph Fidelis Mngwabi na Enoch Marwa Sando.

Mbali na mafunzo hayo maalum, pia Bodi hiyo imekabidhiwa vitendea kazi na miongozo ya kisheria ikiwemo Sheria ya Usajili na Usimamizi wa Wadhamini Sura ya 318, mwongozo wa Katiba na nyaraka nyingine zinazohusu usimamizi wa Bodi za Wadhamini ili ziwe sehemu ya nyezo muhimu zitakazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, David Mpwani mbali ya kuishukuru RITA kwa mafunzo hayo na miongozo amesema kupitia mafunzo hayo yatawawezesha kitimiza majukumu yao kikamilifu na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa lengo la kuhakikisha mali za kanisa zinalindwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.

“Kupitia mafunzo haya yametujenga na kutupa muongozo wa namna ya kutekeleza majukumu yetu kwa ufasaha hivyo waumini wakanisa letu wategemee matokeo chanya yatakayo jenga,kuimarisha na kuinua utume wa kanisa letu,” alisisitiza Mpwani.

RITA imekuwa ikihakikisha upatikanaji wa huduma bora, na za uhakika zenye kuaminika kwa wananchi wote ikiwa ni pamoja na kusimamia, kuratibu huduma muhimu za kisheria zinazohusiana na usajili wa matukio ya maisha ya binadamu ikiwemo vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya ndoa, taraka pamoja na masuala ya ufilisi na udhamini.

About The Author

error: Content is protected !!