March 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

ACT Wazalendo yawasilisha wasiwasi wa hali ya kisiasa UN

 

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (Special Representative of the Secretary General to the African Union and Head of UNOAU), Parfait Onanga-Anyanga, katika kikao kilichofanyika leo Jumanne 10 Machi 2026 katika Ofisi za Ubalozi wa Umoja wa Mataifa jijini Dar es Salaam. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika mazungumzo hayo, Semu aliyekuwa ameambatana na Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa ACT Wazalendo, Wakili Mwanaisha Mndele, alieleza wasiwasi wa chama hicho kuhusu mwenendo wa kisiasa ulioshuhudiwa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, hali ambayo amesema haikuwa ya kuridhisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ACT Wazalendo kwa umma, Semu alieleza kuwepo kwa madai ya ukandamizaji wa demokrasia, uminyaji wa haki za raia na uhuru wa vyombo vya habari, pamoja na tuhuma za wizi wa kura, kukanyagwa kwa haki za kisiasa na vitisho dhidi ya wananchi. Aidha, alidai kuwa kumekuwepo na matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi wanaodai haki zao za kidemokrasia nchini.

Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa mbali na kasoro zilizoripotiwa wakati wa uchaguzi huo, Semu alionyesha masikitiko ya chama hicho na Watanzania kwa ujumla kutokana na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hususan vifo vya baadhi ya raia vilivyotokea katika matukio ya baada ya uchaguzi, ambayo yameacha maumivu kwa familia zilizopoteza ndugu zao.

Katika mazungumzo hayo, Semu alirejea msimamo wa ACT Wazalendo wa kutotambua Tume Huru ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata, iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman.

Chama hicho kimeeleza kuwa Rais ni sehemu ya serikali inayotuhumiwa katika matukio hayo, hivyo kimependekeza kuundwa kwa chombo huru na cha kimataifa kitakachoaminika ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kuwawajibisha wote watakaobainika kuhusika.

Aidha, katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Wakili Mwanaisha Mndele, Semu ameziomba ofisi za Umoja wa Mataifa kulipa uzito suala hilo na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa haki za binadamu na demokrasia nchini Tanzania.

About The Author

error: Content is protected !!