MASHAMBULIZI ya kijeshi ya Marekani na Israel nchini Iran, yamewaondoa maisha ya makumi ya viongozi waandamizi wa taifa hilo la Kiarabu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Kwa mujibu wa taarifa za kijeshi, mashambulizi ya awali yalilenga moja kwa moja safu ya juu ya uongozi wa Iran, yakihusisha viongozi wa kisiasa, kijeshi na washauri wakuu wa serikali.
Jeshi la Israel lilidai kuwa zaidi ya viongozi 40 waandamizi wa jeshi la Iran waliuawa katika mashambulizi hayo.
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema, “operesheni hiyo,” imelenga kuondoa kile alichokiita, “tishio la kiusalama dhidi ya Washington pamoja na kuwapa wananchi wa Iran nafasi ya kuleta mabadiliko ya kisiasa ndani ya nchi yao.”
Miongoni mwa waliofariki dunia, ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei (86), Aziz Nasirzadeh, Ali Shamkhani, Meja Jenerali Mohammad Pakpour na Meja Jenerali Abdul Rahim Mousavi.
Khamenei, alikuwa kiongozi wa pili mkuu tangu mapinduzi ya 1979 baada ya kifo cha Ruhollah Khomeini mwaka 1989 na alikuwa na mamlaka ya juu zaidi nchini Iran.
Naye Aziz Nasirzadeh, aliyezaliwa 1964 katika mji wa Sarab, Kaskazini-Magharibi mwa Iran, alihitimu mafunzo ya urubani na kupata mafunzo ya ziada ya kuendesha ndege za kivita nchini Pakistan.
Aliwahi kuwa miongoni mwa marubani waliotumia ndege za kivita aina ya F-14 wakati wa vita vya Iran na Iraq (1980–1988).
Baada ya vita kumalizika, alishika nyadhifa mbalimbali za kijeshi na kidiplomasia, ikiwemo kuhudumu katika ubalozi wa Iran mjini Rome, Italia.
Amewahi kuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la Anga na baadaye Mkuu wa Wafanyakazi wa Jeshi kati ya mwaka 2009 na 2017.
Kufuatia ushindi wa Rais Masoud Pezeshkian mwaka 2024, Nasirzadeh aliteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi wa Iran.
Ali Shamkhani: Huyu alikuwa mshauri mkuu wa Kiongozi wa Kidini – Ayatollah Khamenei. Alizaliwa 1955 mjini Ahvaz na alikuwa miongoni mwa wanaharakati waliopinga utawala wa Shah kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Mwaka 1975 alishiriki kuanzisha kundi la “Mansouroun” pamoja na Mohsen Rezaei, ambalo baadaye likawa sehemu muhimu ya kikosi cha Revolutionary Guard.
Awali kulikuwa na taarifa zilizodai kuuawa kwake katika mapigano ya awali kati ya Iran na Israel, lakini baadaye ilithibitishwa kuwa alikuwa amejeruhiwa na kunusurika kabla ya kuuawa katika mashambulizi ya hivi karibuni.
Meja Jenerali Mohammad Pakpour, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi (Revolutionary Guard), naye amethibitika kufariki dunia.
Pakpour alishika wadhifa huo, baada ya kuuawa kwa Hossein Salami katika mapigano yaliyotangulia, ambapo alipandishwa cheo kutoka Brigedia Jenerali hadi Meja Jenerali na kuteuliwa kuongoza kikosi hicho.
Katika kipindi chake cha uongozi, alisisitiza mara kwa mara juu ya utayari wa kijeshi wa Iran, akielezea uwezo wa makombora ya nchi hiyo na kuonya kuwa shambulio lolote jipya lingepewa jibu kali.
Alizaliwa mwaka 1961, mjini Arak na kabla ya uteuzi wake aliwahi kuongoza vikosi vya ardhini vya Revolutionary Guard kwa zaidi ya miaka kumi na sita.
Meja Jenerali Mousavi, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Iran, naye aliuawa katika mashambulizi hayo yaliyolenga viongozi wa juu wa kijeshi.
Alizaliwa 1959, katika mji wa Qom na alijiunga na jeshi mwaka 1979. Alipata elimu ya juu katika masuala ya usimamizi wa ulinzi katika Chuo Kikuu cha Supreme National Defense University.
Wakati wa Vita vya Iran na Iraq, Mousavi alipigana katika maeneo ya Kurdistan na Khuzestan akiwa katika kikosi cha mizinga, ambapo aliwahi kujeruhiwa vitani.
Baada ya vita alipanda vyeo mbalimbali hadi kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi mwaka 2017, nafasi aliyodumu nayo hadi Juni 2025.
Mgogoro kati ya Marekani na Iran, tayari umeibua mvutano mkubwa katika ukanda wa Mashariki ya Kati.
Nchi za Ghuba zizoathirika na wimbi jipya la mashambulizi ya Iran, ni pamoja na Qatar, United Arab Emirates na Bahrain.
ZINAZOFANANA
Ikiwa ndio mwanzo unajiunga nasi…
Ayatollah Ali Khamenei: Kiongozi Mkuu wa Iran athibitika kuawa
Kuna dalili za kiongozi mkuu wa Iran kuuawa