Edward Lowassa
NIANDIKE nini kuhusu Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye leo, 10 Februari 2026, imetimia miaka miwili tangu afariki dunia jijini Dar es Salaama na kuzikwa kijijini kwake Monduli. Anaandika Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi, alipata kusema ‘Maisha ya mwanadamu ni hadithi tu. Ewe ndugu yangu kuwa hadithi nzuri kwa hao watakaosimuliwa.’
Nataka niandike kuhusu Lowassa alivyouchangamsha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na alivyokaribia kukiangusha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilichomlea, kumkuza na kumpa fursa ya uongozi. Alikaribia kumfanya mgombea urais, John Magufuli na chama chake kuwa wapinzani.
Mkono wangu ni mzito kuandika kuhusu uchaguzi huo ambao ulitoa taswira ya ubora upinzani nchini ambao ulipata viti vingi vya udiwani, ubunge na kura nyingi za urais.
Lowassa aling’oka CCM baada ya kukatwa kwa kile alichokiita ni ‘zengwe’ kwenye kinyang’anyiro kuomba ridhaa ya kuwania urais kupitia chama hicho tawala na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilichompa fursa ya kuwania nafasi hiyo.
Niandike kuhusu hofu yake ya ukosefu wa ajira kwa vijana alioita ni ‘Bomu linalosubiri kulipuka’? Niandike alivyokuwa anataka serikali ielekeze nguvu zaidi katika maeneo yatakayotoa fursa za uzalishaji mali na kipato kwa kundi hilo?

Nataka kuandika kuhusu alivyokuwa akitaka wafugaji (wamasai) wenzake wabadili mfumo wa maisha kwa kufuga kisasa ili wapate fedha na mafanikio zaidi. mkono unakataa, Nafikiria kuandika alivyokuwa mfuatiliaji wa kila alichokiagiza au anachoagizwa. Akili inagoma.
Ubongo wangu unaniambia niandike kuhusu elimu ambayo kwa miaka mingi tumekuwa tukiambiwa ni ufunguo wa maisha. Lowassa alipokuwa akijinadi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2015 alieleza kipaumbele chake ni
elimu, elimu, elimu.”
Ninawezaje kumsahau Lowassa wakati alisimama kidete kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa shule za kata nchini akiwa waziri mkuu? Shule hizi zimekuwa mkombozi kwa wazazi na wanafunzi. Nani asiyejua faida yake?
Jina lake linasahaulikaje kirahisi wakati angalau amelea usawa wa kielimu hasa kwa wasio na uwezo? zimeongeza uelewa kwa vijana ambao sasa wanahoji na kuchambua kila wanachoambiwa.
Leo, si kwamba namkumbuka Lowassa kwa namna alivyokitikisa kisiasa hadi kuitwa ‘Rais wa mioyo ya watu’ bali alivyofanikiwa kuwathibitishia Watanzania kwa vitendo kuwa elimu ni uti wa mgongo na chachu ya maendeleo ya taifa.
Lowassa aliamini maendeleo hayawezi kupimwa kwa barabara au majengo pekee, bali kwa uwezo wa wananchi kufikiri, kubuni na kushindana katika uchumi wa maarifa.
Kauli yake ya kusisitiza elimu mara tatu ilikuwa ishara ya kuweka kipaumbele kisichopingika kwamba bila elimu, ajira, uchumi na ustawi wa jamii hubaki kuwa ndoto.
Miaka kadhaa baadaye, taswira ya elimu nchini inaonesha hatua na changamoto kwa wakati mmoja. Kwa mfano, mwaka 2026 wanafunzi 937,581 walichaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za serikali, jambo linaloonesha upanuzi wa fursa za elimu ya sekondari.
Kwa upande wa uandikishaji kwa ujumla, viashiria vya kitaifa vinaonesha kiwango cha uandikishaji wa elimu ya awali kupanda hadi karibu asilimia 90, kikilenga kufikia asilimia 91, hatua inayotafsiriwa na wachambuzi kama mafanikio ya sera za kuongeza upatikanaji wa elimu.
Hata hivyo, changamoto bado zipo. Takwimu zinaonesha asilimia 63 ya shule za msingi za serikali zina uhaba wa walimu, huku wastani wa mwalimu mmoja akifundisha wanafunzi 56 badala ya kiwango kilichopendekezwa cha 45.
Kwa jumla, shule za msingi zinahitaji zaidi ya walimu 42,000 wa ziada ili kufikia mahitaji halisi.
Katika elimu ya awali hali ni nzito zaidi – uchambuzi unaonesha mwalimu mmoja akifundisha hadi wanafunzi 120 kwa darasa, idadi inayotajwa kuzidi mara nne kiwango kinachoshauriwa na wataalamu wa elimu ya utotoni.
Kwa mujibu wa wachumi wa elimu, uwekezaji katika shule una faida ya moja kwa moja kiuchumi kwa mtu binafsi na taifa. Tafiti zinaonesha kuwa kila mwaka mmoja wa ziada wa elimu unaweza kuongeza kipato cha mtu kwa wastani wa asilimia 9-11, jambo linalothibitisha hoja ya Lowassa kwamba elimu ni uwekezaji wa maendeleo, si matumizi ya kawaida ya bajeti.
Watafiti wengine wanaonya kuwa pamoja na maendeleo ya kitaifa, bado kuna tofauti za kimkoa katika viwango vya elimu na upatikanaji wake, hali inayohitaji sera zinazolenga maeneo maalum ili kuhakikisha usawa wa fursa.
Aidha, wachambuzi wa elimu ya awali wanasema uwekezaji katika ngazi hiyo hujenga msingi wa ubunifu, mawasiliano na uwezo wa kujifunza wa baadaye, hivyo kupuuzwa kwake kunaweza kudhoofisha ubora wa elimu katika ngazi zinazofuata.
Taswira hii inaonesha ukweli mmoja Tanzania imepanua wigo wa elimu kwa wengi zaidi, lakini mjadala umehama kutoka “upatikanaji” kwenda “ubora”. Hapa ndipo kauli ya Lowassa inapata uzito mpya.
Je, elimu tunayopanua leo inajenga maarifa na ujuzi unaoweza kushindana kimataifa?
Je, tunazalisha wahitimu wanaobadilisha uchumi au wanaotafuta nafasi ndani ya mfumo ule ule?
Maswali haya ndiyo yanayofanya kumbukumbu ya Lowassa iwe zaidi ya historia – iwe kichocheo cha mjadala wa sera.
Kumkumbuka Lowassa leo ni kukumbuka wazo lililokuwa rahisi lakini lenye nguvu: maendeleo ya taifa huanzia darasani. Takwimu zinaonesha hatua zimepigwa, lakini pia zinaonesha kazi iliyobaki.
Urithi wa kauli yake unabaki kuwa changamoto kwa watunga sera na jamii kwa ujumla – kuhakikisha elimu si kauli ya kisiasa tu, bali ni msingi wa vitendo.
Na labda, katika mjadala wa leo kuhusu mustakabali wa taifa, kauli yake bado inasikika wazi:
Elimu, elimu, elimu.
Wakati Watanzania wanakumbuka kwa kusimamia elimu, familia bado inamkumbuka kuwa baba, mume, mjomba, mlezi uliyoondoka duniani ikiwa bado wanahitaji mawazo, busara, ujasiri na uthubutu wako.
MUNGU AILAZE ROHO YAKE MAHALI PEMA PEPONI AMIIN
ZINAZOFANANA
Tanzania kujisogeza Ulaya, Zungu apiga hodi Serbia
TAMISA yataja maeneo 20 muhimu ya ‘kupiga pesa’ kwenye madini
Lissu alalamika kuchelewa kesi yake