February 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Lissu alalamika kuchelewa kesi yake

 

TUNDU Antipas Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameilalamikia Mahakama Kuu, Masjala ndogo ya Dar es Salaam, kumcheleweshea kesi yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza mahakamani leo Jumatatu, tarehe 9 Februari 2026, Lissu amesema, mpaka sasa ametimia miezi 10 tangu alipokamatwa tarehe 9 Aprili mwaka jana na kushtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, tarehe 10 Aprili mwaka jana.

Lissu anayekabiliwa na kesi Uhaini, Na. 19605/2025, ameeleza kuwa Mahakama inapaswa kuwajibuika, ili kumaliza kesi yake mapema. Akaongeza, hajajipeleka magereza, amepelekwa na watawala na hivyo, kwamba “…haki iliyocheleweshwa, ni haki iliyokiukwa.”

Alisema, ni wajibu wa Mahakama kuhakikisha kesi yake inasikilizwa haraka. Alisema, “Katiba yetu inaelekeza Mahakama ziendeshe mashauri kwa namna ambayo haitachelewesha haki. Ndivyo Ibara ya 147 ya Katiba inavyosema.”

Lissu amenukuu kifungu cha 5 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kinachosema mashauri yanaendeshwe kwa haraka.

Tundu Lissu akiingia mahakamani

Lissu ametaja kuwa changamoto za kudorora kwa mwenendo wa shauri dhidi yake unatokana na kuendeshwa kwa mtindo wa vikao “Tatizo lipo kwenye utaratibu wa session ndio tatizo na hilo ni tatizo la wanaoamua kesi iendeshwe kwa njia ya session”

Mwanasiasa huyo ameisomea mahakama hiyo kilichoandikwa kwenye Ripoti ya Haki Jinai ya 2-23 ukurasa wa 17 na 18 kuhusu vikao vya Mahakama Kuu, kwamba ripoti imesema, uendeshaji wa mashauri kwa njia ya vikao huchelewesha mashauri hayo.

“Kati ya mashauri 2000 ni mashauri 700 tu ndio yalisikilizwa pekee kwa mtindo wa session. Hivyo basi, uendeshaji wa kesi kwa kutumia session unaamuriwa na Jaji Mkuu zikiisha siku tunasubiri aseme tena ndio maana zimepita siku 88 bila kesi hii kuendelea hadi atakapopanga tena huyo Jaji Mkuu,” alifafanua.

Ameeleza kuwa ucheleweshaji huu sio kosa la majaji wala mawakili wa Serikali ni kosa la utaratibu uliowekwa uliwekwa na mahakama.

Akaongeza, “Leo hapa High Court (Mahakama Kuu) Dar es Salaam, kuna majaji wakutosha. Lakini ili kesi yangu isikilizwe lazima Jaji atoke Songea, mwingine Mtwara sijui na lazima walipwe, usafiri, chakula na kila kitu.

“Usipowalipa kesi haiendelei na mimi mtuhumiwa nateseka huko jela. Walishindwa nini kuwapangia majaji wa hapa ili kesi isikilizwe kila siku,” alihoji Lissu.

Kwa mujibu wake, “Zamani majaji walikuwa wachache sana lakini siku hizi kila mkoa kuna majaji. Nashangaaa mambo haya kwa utaratibu huu sasa.”

Lissu amedai kuwa shtaka la uhaini ndio kosa kubwa zaidi nchini. “Hili ni kosa la kipekeee, angalieni Ibara ya 28(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndio kosa pekee la jinai lililotajwa kwenye Katiba kwasababu sio kosa la kawaida.”

“Kama hiyo ndio hoja kosa hili pia la uhaini linapaswa kuwa na kipaumbele, maana ni tofauti na makosa mengine yote,” ameeleza.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini mezitaja kesi mbili za uhaini zilizowahi kutokea nchini na kwamba kesi yake ni ya tatu tokea taifa hili lipate uhuru.

Alisema, “Kesi ya Grey Likungu, miaka 56 iliyopita, ilikuwa na washitakiwa 9 lakini ilichukua miezi 6 tu hadi kufika mahakama ya rufani.

“Kesi nyingine, ni ya Khatib Gandi na wenzake 18 kutoka Mahakama Kuu hadi Court of Appeal (Mahakama ya Rufani), kuanzia ilipoanzia hadi ilipoishia ilichukua miezi 14 na mashahidi 140. Sisi tuna miezi 10 tumemaliza mashahidi watatu tu.”

Lissu anasema: “Vyovyote itakavyokuwa kesi hii inachukuliwa kama kesi ya kawaida ya jinai. Haiwezi chukuliwa poa hata kidogo lazima hili lieleweke vizuri.

“Kwa utaratibu huu tutafika mwaka 2030 kama mtakuwa hamjastaafu bado kwa spidi hii ya miezi 10 mashahidi watatu. Sasa kesi ya Grey Likungu Mataka ilisikilizwa na jaji mmoja na kesi ya Khatib Gandi Ilisikilizwa na jaji mmoja pia. Kesi ya tatu Jaji Mkuu anasema mmoja hawezi ndio maana anawateua muwe watatu kusikiliza kesi hii,” anaeleza kwa njia ya msisitizo.

Kwenye kesi hii, Lissu anasema, “Jaji mkuu asipowatumieni hela hamji. Kesi hii ina ugumu gani hadi muwe watatu. Ni kunicheleweshea haki yangu tu. Hakuna lingine.”

About The Author

error: Content is protected !!