February 2, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Venezuela yawaachia wafungwa zaidi ya 300 wa kisiasa

NI takribani watu 300 wanaotambuliwa kama “wafungwa wa kisiasa” wameachiliwa nchini Venezuela ndani ya siku 30 tangu kupinduliwa na kutekwa kwa Rais Nicolas Maduro na majeshi ya Marekani mwezi mmoja uliopita. Anaripoti Mohammed Khelef, kutoka DW Ujerumani … (endelea).

Shirika la haki za binaadamu, Foro Panel, limethibitisha hadi sasa kuachiliwa huru kwa wafungwa 334 tangu serikali ilipotangaza kuanza kwa hatua hiyo mwanzoni mwa Januari, wafungwa 33 kati yao wakiwa wameachiwa siku ya Jumapili (2 Februari).

Kuachiliwa kwa watu hao, kunakuja baada ya rais wa mpito wa Venezuela, Delcy Rodriguez, kutangaza rasimu ya “sheria ya msamaha” siku ya Ijumaa (30 Januari), kwa ajili ya mamia kwa maelfu ya wafungwa.

Rais Rodriguez, ameeleza kuwa gereza la Helicode lililopo katika mji mkuu (Caracas), sasa lingegeuzwa kuwa kituo cha michezo na shughuli za kijamii.

Makamu rais wa shirika la Foro Panel, Gonzalo Himiob, aliandika kwenye ukurasa wa X kwamba “kila hatua kuelekea uhuru na ukomeshaji wa ukandamizaji ni muhimu.”

Maafisa wa serikali, ambao wanakanusha kuwashikilia wafungwa wa kisiasa wakidai waliofungwa wametiwa hatiani kwa uhalifu, walisema idadi ya walioachiliwa hadi sasa ni zaidi ya 600, ingawa idadi hiyo inaonesha kuwajumuisha walioachiliwa kabla.

Miongoni mwa walioachiliwa siku ya Jumapili, ni pamoja na mwanaharakati wa haki za binaadamu, Javier Tarazona, ambaye alikamatwa mwaka 2021.

“Baada ya siku 1,675, miaka minne na miezi saba, hatimaye siku tuliyokuwa tukiiomba imefika. Kaka  yangu Javier Tarazona yuko huru. Uhuru wa mtu mmoja ni matumaini kwa wote.” Aliandika kaka wa mwanaharakati huyo, Jose Rafael Tarazona, aliandika kupitia ukurasa wa X.

Tarazona ni mkurugenzi wa shirika la FundaRedes, ambalo linafuatilia matendo ya ukandamizaji yanayotendwa na makundi yenye silaha ya Kolombia na jeshi la Venezuela mpakani mwa nchi hizo.

Alikamatwa kwa tuhuma za ugaidi na kula njama dhidi ya taifa hilo la Amerika Kusini.

Uachiliwaji wafungwa umekuwa ukienda kwa kasi tangu Venezuela ilipotangaza sera ya uachiaji mnamo 8 Januari, kufuatia kutekwa nyara kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro, na jeshi la Marekani, mapema mwezi uliopita.

Maelfu bado wangalimo magerezani

Shirika la haki za binaadamu la Foro Penal linasema zaidi ya watu 700 bado wanashikiliwa kwenye gereza la Helicoide pekee baada ya kuachiliwa zaidi ya 334 wa sasa.

Lakini serikali bado haijasema ni kiasi gani cha wafungwa wamesalia gerezani na wangapi na wapi wataachiliwa.

Hata hivyo, familia za wafungwa hao zinasema, mchakato wa uachiwaji ndugu zao umekuwa ukienda kwa kasi ndogo, huku wakitaka mashitaka dhidi yao yafutwe moja kwa moja.

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na kiongozi wa upinzani wa Venezuela, Maria Coria Machado, ambaye wenziwe kadhaa wako gerezani, amekuwa akipigania kuachiliwa kwa.

Miongoni mwa watu mashuhuri ambao bado wako gerezani ni pamoja na mwanasiasa wa upinzani, Juan Pablo Guanipa, mwanasheria Perkins Rocha na kiongozi wa chama cha upinzani cha Voluntad, Freddy Superlano.

Katika ripoti yake ya mwaka 2022, Umoja wa Mataifa ulisema wafungwa kwenye gereza la Helicoide walikuwa wakiteswa vibaya, tuhuma iliyokanushwa na serikali.

About The Author

error: Content is protected !!