Vincent Mughwai Lissu
VINCENT Mughwai Lissu, mdogo wa mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anatolea ufafanuzi wa kinachoitwa, “upigaji wa fedha za michango ya kaka yake.” Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza na MwanaHALISI Online, leo Alhamisi, Vincent amesema, michango iliyokusanywa kwa ajili ya kaka yao, haikukusanywa na Chadema wala viongozi wake.
“Ile kazi ilikuwa inafanywa na familia. Haikufanywa na Chadema wala viongozi wake. Akaunti zilizokuwa zikitumika, zilikuwa za kaka yetu, Alute Mughwai, siyo katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika.
Siyo naibu katibu mkuu mkuu, Aman Golugwa, wala siyo makamu mwenyekiti, John Heche,” amesisitiza Vincent na kuongeza, “Hivyo hayo yanayoelezwa mitandaoni, yote ni uwongo mtupu.”
Kwa mujibu wa Vincenti, mmoja wa wasaidizi wa Lissu aliyemtaja kwa jina la Fredrick Mbwambo, alikwenda kwa Alute na kumuomba aruhusu kuendeshwa michango kwa ajili ya kumsaidia Lissu, katika kipindi hiki kigumu anachopitia.

Lissu yuko gerezani tokea Aprili mwaka jana, akituhumiwa kwa makosa ya uhaini, ingawa yeye na chama chake wanasema, mashitaka yanayomkabili yanatokana na mashinikizo ya kisiasa.
Anasema, “Fred (Fredrick) alimueleza kaka yetu Alute, kwamba kuna marafiki wa Lissu, wanataka kumchangia, ili kufunga mwaka pamoja naye.
“Baada ya kumkubalia ombi hilo, Fred aliomba achiwe simu zilizokuwa zinapokea fedha hizo, ili kumsaidia kufanya mrejesho kwa wanaochangia au wanaotaka kuchanga.”
Hata hivyo, Vincent anasema, baadaye ikaja kugundulika kwamba fedha zimeibiwa na aliyezichukua kwa njia ya kuzihamisha, ikiwamo kujihamishia mwenyewe, ni Fredrick Mwambo.
Anasema, “Uchunguzi uliofanywa na Alute, kwa ushirikiano na makampuni ya simu, umethibitisha kuwa fedha hizo, zimechukuliwa na Fredrick,” anaeleza Vincent.
Kauli ya Vincent imekuja siku moja baada ya jeshi la polisi mkoani Arusha, kueleza kuwa linamshikilia Mbwambo, mwanachama wa Chadema, kwa tuhuma za wizi wa fedha za michango ya Lissu.
Mwishoni mwa mwaka jana, baadhi ya wafuasi wa chama hicho, walianzisha harambee ya kumchangia kiongozi wao, anayeshikiliwa katika Gereza la Kuu la Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Akifafanua hoja yake, Vincent anasema, “Fredrick ndiye aliyekuwa anakusanya michango hiyo, kupitia akaunti za simu za Alute Mughwai,” – kaka mkubwa wa Tundu.
Anasema, michango hiyo, haikuwahusisha viongozi wa Chadema, na kwamba yanayoiripotiwa kwenye vyombo vya habari, juu ya chama hicho, yanalenga kukichafua.
“Kuna kampeni kubwa ya kutaka kuingiza Chadema katika jambo hili. Ukweli ni kwamba michango ilikusanywa na familia. Iliratibiwa na familia na yaliyotokea, yanahusu familia,” alifafanua.
ZINAZOFANANA
Mbaroni kwa kuiba fedha za Lissu
Miezi mitatu baada ya vurugu za 29 Oktoba: Familia bado zinasubiri miili
Tamko la ACT Wazalendo juu ya maamuzi ya kesi ya uchaguzi