January 29, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mbaroni kwa kuiba fedha za Lissu

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia Fredrick Mbwambo, mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa tuhuma za wizi wa fedha za michango zilizokuwa zikikusanywa kwa ajili ya Mwenyekiti wa chama hicho aliyeko gerezani kwa tuhuma za uhaini, Tundu Lissu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Januari 28, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, mtuhumiwa huyo alikamatwa jana tarehe 27.01.2026 kufuatia malalamiko rasmi yaliyowasilishwa na Alute Mughwai baada ya kubainika kutokea kwa wizi wa fedha hizo.

“Ufuatiliaji wa awali umeonesha kuwa ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za kampuni tofauti za simu na inadaiwa zilihamishiwa kwenye namba mbili za simu moja ikiwa ni ya kampuni ya Tanzania na ya pili ni kampuni ya simu ya nchi jirani”, imeeleza taarifa hiyo.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa jalada la shauri hilo limekwishafunguliwa na uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini kiasi halisi cha fedha kilichoibiwa.

Aidha, Polisi mkoani Arusha wamesisitiza kuwa jitihada za kuwatafuta watuhumiwa wengine wanaodaiwa kushirikiana na Mbwambo katika mtandao huo wa wizi zinaendelea, pamoja na kutafuta vielelezo kwa hatua zaidi za kisheria.

About The Author

error: Content is protected !!