January 20, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

AG Zanzibar aweka mapingamizi kesi za Uwakilishi

Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban

 

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar anayelalamikiwa kwenye kesi za kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 ameweka mapingamizi katika kesi nane zilizotajwa leo. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Akitumia jopo la wanasheria kutoka ofisi yake likiongozwa na Said Salim Said, ameiambia Mahkama Kuu ya Zanzibar kuwa tupo tayari kwa usikilizaji wa mapingamizi hayo waliyoweka.

Alitoa maelezo hayo mbele ya Jaji Mohamed Ali Shein ambaye awali alieleza kufikia hatua ya kesi kupangiwa majaji, ina maana taratibu za awali za ufunguaji zimekamilika na kwamba sasa usikilizaji unaanza.

Jaji Shein alisema ameita kesi hizo kwa pamoja leo zikihusu mashauri manane ili kuelewana namna kazi itakavyofanyika.

Alikubali ombi la pande zote kwamba ni vema kesi zikiunganishwa na kusikilizwa kwa pamoja kwa kuwa mazingira yake yanafanana.

Mwanasheria Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Omar Said Shaaban, anayewakilisha wanachama waliokuwa wagombea kwenye uchaguzi uliofanyika kwa siku mbili tarehe 29-30 Oktoba 2025, alieleza mahkamani kuwa ni busara usikilizaji ukafanywa pamoja kwa kuwa yanayoelezwa kwa shauri moja yanalingana na yalioko shauri jengine.

Baada ya Mwanasheria Said Salim anayemwakilisha AG Zanzibar kueleza kuhusu mapingamizi ya upande wao, Jaji Shein aliakhirisha kesi hizo na kupanga tarehe 24 mwezi ujao kuanza usikilizaji wa mapingamizi hayo.

Jaji Shein amepangiwa mashauri ya majimbo ya Pangawe, Malindi, Mwanakwerekwe, Kiembesamaki, Chaani, Chumbuni, Mkwajuni na Makunduchi.

Mbali na Mwanasheria Mkuu wa SMZ, walalamikiwa wengine katika kesi hizo ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar [ZEC), taasisi iliyoandaa na kusimamia uchaguzi mkuu unaolalamikiwa kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu.

Taarifa kutoka Chake Chake, kisiwani Pemba, zinaeleza kuwa Mahkama Kuu ya Zanzibar mbele ya Jaji Haji Suleiman Tetere, ilianza jana kusikiliza mapingamizi yaliyowekwa na upande wa walalamikiwa katika kesi za majimbo manane.

Majimbo hayo ni Kojani, Micheweni, Wawi, Chake Chake, Chonga, Mkoani na Kiwani ambako Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla, kuwa mshindi.

Pia malalamiko yamefunguliwa kuhusu uchaguzi wa diwani Shehia ya Kibirinzi, Wilaya ya Chake Chake, Pemba.

Bado haijafahamika mashauri tisa ya kupinga uchaguzi wa uwakilishi kisiwani Unguja yamepangiwa jaji gani.

ACT Wazalendo kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wake, Omar, imefungua mashauri kwa majimbo 25 ya uwakilishi na 33 ya ubunge.

Wakati kesi za uwakilishi zinaanza kusikilizwa mbele ya Mahkama Kuu ya Zanzibar, zile za uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano zimeingia utata kufuatia hoja ya Mwanasheria Mkuu wa SMT kuwa mahkama hiyo haina mamlaka na uwezo wa kuzisikiliza.

Hoja hiyo ilikamilika kusikilizwa wiki iliyopita; na Jaji Haji Tetere amepanga kutoa uamuzi mdogo kuhusu hoja hiyo hapo tarehe 27 mwezi huu.

About The Author

error: Content is protected !!