Rais Nicolas Maduro
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amesema Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro, atafikishwa mahakamani nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).
Amesema, Maduro atakabiliwa na mashitaka nchini Marekani, kutokana na tuhuma kadhaa zinazomkabili.
Amekiri kuwa Maduro na mkewe, Cilia Flores, wamekamatwa baada ya mashambulizi makubwa ya kijeshi nchini mwao na wanashikiliwa nchini Marekani.
Kwa mujibu wa Rubio, hakutakuwa na hatua zaidi zitazochukuliwa dhidi ya Venezuela kufuatia kukamatwa kwa Maduro.
Seneta Mike Lee amesema, baada ya mazungumzo yake na Rubio, amehakikishiwa kuwa hakutakuwa na hatua zaidi dhidi ya Venezuela baada ya Maduro kuwa mikononi mwa Marekani.
Aliongeza, mashambulizi ya Marekani yalifanywa ili “kulinda na kuhakikisha wale wanaotekeleza amri ya kukamatwa wanashirikiana kwa ajili ya usalama.”
Awali, Lee alisema kupitia chapisho lake kwenye X: “Natarajia kujua kama, na ikiwa kuna sababu za kikatiba zinazoweza kueleza hatua hii bila kuwa na tangazo la vita au idhini ya kutumia nguvu za kijeshi.”
Mapema Makamu wa Rais wa Venezuela, Delcy Rodríguez, alisema serikali yake haijui mahali alipo Rais Maduro wala mkewe, na kuitaka Marekani kutoa “uthibitisho wa uhai wake.”
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa, Rodríguez alidai kuwa serikali ya Venezuela ina wasiwasi mkubwa kuhusu hatima yao.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la Venezuela, Rodríguez alisema, “Tunaitaka serikali ya Marekani kutoa uthibitisho wa uhai wa Rais Maduro na Mama wa Taifa. Rais alikuwa tayari ametuonya kuwa hali kama hii inaweza kutokea.”
Rodríguez aliongeza kuwa raia wameanza kufahamu kwamba rais alikuwa ametoa maelekezo ya wazi kwa vyombo vya ulinzi kuanza kutekeleza mipango yote ya kulinda taifa kwa mshikamano kamili.
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino, amesema serikali inaendelea kukusanya taarifa kuhusu watu waliopoteza maisha na waliojeruhiwa, huku akidai kuwa mashambulizi hayo pia yalilenga maeneo ya raia.
Amesema, Venezuela itapinga vikali uwepo wa majeshi ya kigeni nchini humo.
Marekani imefanya mashambulizi makubwa maeneo ya kijeshi mjini Caracas na sehemu nyingine za nchi, huku mashinikizo ya kisiasa na kiusalama yanayoongezeka kwenye nchi hiyo, yakitishia kuathiri maisha ya raia na uchumi wa ndani.
ZINAZOFANANA
Nchi sita zapinga kukamatwa kwa Rais wa Venezuela
Trump amuonya kiongozi wa muda wa Venezuela
Nicolás Maduro, ang’olewa madarakani, ashikiliwa Marekani