December 30, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

M23 yajipanga kuangusha serikali DRC

 

CORNEILLE Nangaa, kiongozi wa muungano wa waasi wa AFC/M23, amesema kuwa kundi lake limepanga kushinda vita, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

“Hatuna lengo jingine isipokuwa kushinda vita ya “kuikomboa DRC nzima,” amesisitiza Nangaa.

Kauli ya kiongozi huyo imekuja, wakati hali ya usalama mashariki mwa DRC ikiendelea kuzorota, huku mazungumzo ya amani yakionekana kukwama.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa AFC/M23 uliofanyika Jumatatu mjini Goma, Nangaa alisema, “mwaka 2026 utakuwa mwaka wa ushindi” kwa harakati zao.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kutathmini hali ya mwaka uliopita na kupanga mikakati ya mapambano kwa mwaka ujao.

Katika taarifa ya kundi hilo, Nangaa alisema, AFC/M23 inalenga kuimarisha jeshi lake na kulijenga upya ili liwe “mfano wa jeshi la baadaye, lililojengwa vizuri, lenye nidhamu na lisilo na vitendo vya kihalifu.”

Aliongeza kuwa wanajiona kama “mwanga” utakaoangaza mustakabali wa Congo, akitumia taswira ya jua linalochomoza Mashariki.

Wiki iliyopita, AFC/M23 waliuteka mji wa Uvira, huku Serikali ya DRC ikiendelea kudai kuwa wapiganaji hao wanaungwa mkono moja kwa moja na jeshi la Rwanda.

Ingawa Rwanda imekuwa ikikanusha vikali tuhuma hizo, lakini madai hayo yamerudiwa majuzi na msemaji wa zamani wa jeshi la DRC, Meja Jenerali Sylvain Ekenge.

Kwa upande wake, Ekenge alikubaliana na kauli ya Nangaa kuhusu kuendelea na mapigano, akisema: “Lazima tupigane… lazima tupigane hadi tukomboe maeneo yote yaliyotekwa na M23.”

Kauli hizi zinaonyesha kuwa pande zote mbili zinaandaa mikakati ya kijeshi badala ya kisiasa.

Hali hii inakuja wakati mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Congo na waasi wa M23, yanayoendelea mjini Doha, yamechukua zaidi ya miezi saba bila kuleta matokeo ya wazi.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa usalama, mazungumzo hayo sasa yanaonekana kusimama kabisa, huku mapigano yakiongezeka.

Mapema mwezi huu, jina la Nangaa pia lilitajwa katika muktadha wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Washington kati ya Rais wa DRC, Félix Tshisekedi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, mbele ya Rais wa Marekani Donald Trump.

Makubaliano hayo yalilenga kumaliza vita na kulisambaratisha kundi la waasi la FDLR, linalopinga serikali ya Rwanda na kufanya shughuli zake mashariki mwa Congo.

About The Author

error: Content is protected !!