ASKOFU Kanisa Katoliki, Jimbo la Kayanga, mkoani Kagera, Mhashamu Almachius Vincent Rweyongeza, amewakemea watu na makundi katika jamii ya leo yanayotumia nguvu, risasi na mabomu ya machozi kwa sababu ya kushindwa hoja, akiwafananisha na akina Herode waliokataa kumpokea Yesu Kristo, Mfalme wa Amani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).
Katika homilia yake, Askofu Rweyongeza amesema, watu wanaoshindwa katika hoja, tafakari, midahalo na maridhiano, mara nyingi hukimbilia matumizi ya nguvu ili kunyamazisha sauti za wanaotumia hoja na fikra.
Amesema, kundi la kwanza la watu wasiompokea Yesu ni akina Herode, akiwataja kuwa ni watu wenye ubinafsi, uchu wa madaraka na ukatili.
Amesema, “Watu hawa hawapendi kushauriwa, kuonywa wala kusemwa, na badala yake hutumia nguvu pale wanaposhindwa hoja.”
Askofu huyo amesema kundi la pili ni Mafarisayo, aliowataja kuwa ni wanafiki wanaotumia dini kama kifuniko cha kufanikisha ajenda binafsi.
Amesema, watu hawa hujifanya wacha Mungu lakini kwa vitendo wakijihusisha na vitendo vya ufisadi, unyonyaji na uharibifu wa taasisi za dini.
Amelitaja kundi la tatu kuwa la Yuda Iskariote, watu wanaomsaliti Yesu kwa busu; wanaoonekana watakatifu kwa nje lakini ndani wakitafuta namna ya kunasa, kuharibu au kunufaika binafsi kupitia mali, sadaka na rasilimali za kanisa.
Akizungumza katika Homilia yake, Askofu Rweyongeza amelitaja kundi la nne ni la akina Pilato. Amesema, hawa ni watu wanaoujua ukweli, lakini huchagua kunawa mikono na kukaa kimya.
“Hawa huruhusu dhuluma, uonevu na mauaji ya haki kufanyika, bila kuchukua msimamo wa wazi,” amefafanua kiongozi huyo.
Amelitaja kundi la tano kuwa ni la wale aliowafananisha na Wayahudi waliomsulubisha Yesu, akiwataja kuwa ni watu wanaodhalilisha, kuumiza, kupora mali za waathirika, kuwanyonya wanyonge na hata kuwanyima yatima haki zao baada ya vifo vya wazazi wao.
Askofu Rweyongeza amesema, makundi hayo bado yapo katika jamii ya leo na yanaendelea kutokumpokea Yesu kwa sura mbalimbali, licha ya kusherehekea Krismasi na kutambua kuzaliwa kwake.
Hata hivyo, Mhashamu Askofu Rweyongeza amesema, bado wapo watu wanaompokea Yesu kwa matendo yao, kwa kuishi katika haki, amani, maridhiano na kulinda utu wa binadamu, jambo ambalo amesema ndilo msingi wa ujumbe wa Krismasi.
Kanisa Katoliki nchini, limekuwa mstari wa mbele kuhubiri upendo, huku likiweka mbele msingi wa kutangulizwa haki, badala ya kuhubiri amani, likieleza kuwa “Bila Haki, Hakuna Amani.”
ZINAZOFANANA
Dk. Mohamed aendeleza mageuzi katika jamii ya Mtambwe
TMA yatahadharisha kuwapo mvua kubwa
Watumishi TEMESA wafutwe kazi – Mwigulu