December 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

SADC watua nchini kushughulikia mgogoro wa kisiasa

 

MJUMBE maalum wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Dk. Naledi Pandor, aliyeshughulikia mgogoro nchini Tanzania, ametinga nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam …( endelea).

Dk. Pandor, aliteuliwa na SADC kuwa mwalikishi wake maalum wa kushughulikia mgogoro wa kisiasa nchini Tanzania, katika mkutano wa viongozi wa jumuiya hiyo, uliofanyika kwa njia ya mtandao, Jumatatu iliyopita.

Mkutano wa SADC ulikuwa chini ya uenyekiti wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Tanzania iliwakilishwa na makamu wa rais, Balozi Emmanuel Nchimbi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Tanzania, Dk. Pandor, aliwasili nchini jana na kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Zanzibar.

Dk. Grace Naledi Mandisa Pandor, aliteuliwa na SADC kuwa mwakilishi wake katika mgogoro wa Tanzania, ni mmoja wa wanadiplomasia wanaoheshimika sana barani Afrika.

Aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini, kati ya 30 Mei 2019 hadi 30 Juni 2024.

Haya yanajiri siku moja baada ya gazeti la MwanaHALISI kuripoti kuwa SADC, imemteuwa mwanadiplomasia wake huyo, kushughulikia mgogoro huo wa kisiasa nchini, uliotokana na maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka huu.

Katika maandamano hayo, maelfu ya watu wameripotiwa kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhumiwa.

Hata hivyo, idadi kamili ya watu waliofariki dunia katika maandamano hayo, bado haijapatikana kutokana na hatua ya Serikali, kugoma kutaja idadi halisi ya watu waliokufa.

SADC ni miongoni mwa taasisi za kimataifa na kikanda, zilizogoma kuutambua uchaguzi mkuu wa Tanzania, kuwa ni uchaguzi huru na haki.

Ujumbe wa waangalizi kutoka SADC waliokuwapo nchini wakati uchaguzi unafanyika walisema, uchaguzi huo, umeshindwa kukidhi viwango vya kidemokrasia vya jumuiya hiyo.

“Uchaguzi huu, ulitawaliwa na vitisho dhidi ya viongozi wa upinzani, vikwazo vya uhuru na ukosefu wa uwazi wakati wote wa mchakato wa uchaguzi. Katika maeneo mengi, wapiga kura hawakuweza kueleza kwa uhuru mapenzi yao ya kidemokrasia.”

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa uchaguzi huo “ulipungukiwa na matakwa ya Kanuni na Miongozo ya SADC ya Kusimamia Uchaguzi wa Kidemokrasia (2021)”, kigezo cha uchaguzi huru, wa haki, na wa kuaminika miongoni mwa nchi wanachama.

Ujumbe huo vilevile uliripoti kuhusu kutengwa kwa wagombea wa upinzani kwa kukamatwa, na kupewa vitisho – ikiwa ni pamoja na kuwekwa kizuizini kwa kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, anayetuhumiwa  kwa uhaini.

Aidha, gazeti la MwanaHALISI liliripoti kuwa Jumuiya ya Madola (Commonwealth), tayari imeijulisha serikali ya Tanzania, kwamba imebakisha miezi mitatu, kabla ya kuondolewa kwenye jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Madola yenye wanachama kadhaa, wakiwamo Uingereza, huenda ikachukua uamuzi wa kuisimamisha uanachama wa Tanzania, kutokakana na madai ya kutompa ushirikiano, mjumbe wake maalum wa kushughulikia mgogoro wa Tanzania, Dk. Lazarus Chakwera, rais mstaafu wa Malawi.

Mkutano wa kuijadili hatma ya Tanzania, unatarajiwa kufanyika tarehe 7 Machi 2026, mjini London. Uingereza ni miongoni mwa nchi ya tatu zenye uwekezaji mkubwa nchini.

Nayo ripoti mpya ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu ulimwenguni la Amnesty International, limedai kuwa wakati wa maandamano ya 29 Oktoba, kulifanyika mauaji, majeruhi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu vilitendeka na kutaka uchunguzi huru na wa kina.

“Vikosi vya usalama vya Tanzania vilitumia nguvu kubwa kupita kiasi, ikiwemo mauaji, katika kuzima maandamano ya uchaguzi yaliyofanyika kati ya tarehe 29 Oktoba na 3 Novemba 2025,” inaeleza ripoti ya Amnesty International.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa hatua hizo zilionesha kiwango cha kutisha cha kutojali haki ya uhai na uhuru wa kukusanyika kwa amani.

Kwa mujibu wa Amnesty, mamia ya watu wanadaiwa kuuawa au kujeruhiwa wakati wa operesheni za vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Shirika hilo linasema matumizi ya nguvu hayakuwa ya uwiano na yalikiuka viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

Katika kukusanya taarifa zake, Amnesty International ilifanya mahojiano na watu 35, wakiwemo manusura wa kupigwa risasi, waliopata majeraha kutokana na mabomu ya machozi, mashuhuda wa matukio, mawakili waliowatetea waandamanaji waliokamatwa, wahudumu wa afya waliowahudumia majeruhi, pamoja na ndugu wa watu waliouawa.

Taarifa kamili soma gazeti lako la MwanaHALISI linalopatikana mtaani wiki hii – Mhariri.

 

About The Author

error: Content is protected !!