December 17, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mwelekeo wa Chaumma ni upi?

 

MWELEKEO wa sasa wa chama cha ukombozi wa umma (CHAUMMA), bado umebaki kuwa ule ule wa kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba. Anaandika George Kabadi, Dar es Salaam … (endelea).

Ni mwelekezo wa kutojua itikadi, sera na falsafa yake kwa wananchi. Ndio! Chauma kama chama cha siasa, hakijui kisimame wapi? Kisimame katika itikadi, sera na falsafa ipi, kwa kuwa kabla ya uchaguzi haikuwa ajabu kukutana na habari za kutetea Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kukiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Aidha, wakati wa uchaguzi, tulikuwa tunasikia kauli za Hashim Rungwe, mwenyekiti wa chama hicho, akizungumza juu ya utamu wa ubwabwa.

Baada ya uchaguzi tunamkuta mmoja wa wanachama wake, Yericko Nyerere, akiibuka na kuzungumzia anachodai “kitachoendelea Chadema.” Haishii hapo. Anaendelea kuipamba serikali mara nyingi, kuliko anavyokizungumzia chama chake – Chauma.

Ukiwa na furaha iliyozidi, usishawishike kuivunja nyumba uliyoijenga kwa raslimali, muda na fedha, kwa kuwa baada ya furaha, kitachofuata ni aibu.

Salum Mwalimu, Aliyekuwa Mgombea Urais wa Uchaguzi Mkuu 2025 kupitia Chaumma

Chaumma inaangushwa na ujuaji na matarajio ya baadhi ya watu ndani ya chama hicho, kuamini kwamba serikali ya CCM, ipo upande wao na wanaweza kukumbukwa kwenye teuzi mbalimbali.

Hivyo ndivyo wanavyofikiri. Hawajang’amua kwamba tayari tumetapeliwa. Wanasiasa wa aina hii, ni wa ajabu sana. Huamini katika kubebwa. Siyo katika ushawishi wao wa kisiasa.

Huu ndio msingi mpaka sasa, Chaumma haijaonyesha kuguswa na yaliyotokea 29 Oktoba – siku ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani – hadi siku nyingine tatu zilizofuata.

Hawajaguswa na watu waliojeruhiwa. Watu waliofariki dunia, miili kutopatikana; na au mali za umma na binafsi zilizoharibika.

Chaumma hakijawahi kulaani wala kutoa pole kwa waathiriwa. Kimeishia kuzomea waandamanaji na kutetea serikali.

Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe

Hapa ndipo najiuliza, hatima yao kwa wananchi ni ipi? Je, wananchi waliopotza ndugu na wapendwa wao, watakiamini Chaumma?

Chaumma isiyo na sauti mbele ya maslahi na fursa zinazowahusu viongozi wa chama hicho, itawezaje kuaminika?

Ikiwa kuna watu wengi wamejeruhiwa 29 Oktoba, wamepoteza maisha mali nyingi zimeharibika, bado Chaumma kama taasisi ya umma iliyoshiriki moja kwa moja katika mchakato wa uchaguzi, haikuhunishwa na kilichotokea, basi safari yake itakuwa imefika mwisho.

Yawezekana wameamua kuchangua njia ilizopitia Tanzania Lebour Party (TLP), baada ya Augustino Mrema, kuondoka NCCR- Mageuzi na kujiunga na chama hicho.

Wengi waliomfuata Mrema katika TLP, walikuwa watu waliokubali kudanganywa na watawala – kama ambavyo wamedanganywa waliondoka Chadema kwenda Chaumma.

Baadhi yao, walihamia TLP, bila mioyo yao kuhama NCCR-Mageuzi. Matokeo yake, wakatumia muda mwingi kuijadili NCCR-Mageuzi, badala ya kujenga chama chao.

Badala yake, makada wa Chaumma, wamekuwa wakikemea na kukebehi matamko ya baadhi ya taasisi na mashirika kama Baraza la Maakofu Katoliki (TEC), Chadema, Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na wengineo.

Hivyo basi, binafsi siioni Chaumma ikiwa chaguo la wananchi kutokana na aina ya siasa zake za kuwa kivuli cha dola; mtu yeyote mwenye malengo hawezi kubaki kwenye safari ya kuelekea 2030.

Mwandishi wa makala hii, G e o r g e Kabadi, mkulima na mwanachama mwandamizi wa TANU.

About The Author

error: Content is protected !!