November 28, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Hatufahamu kesi ya Lissu itaendelea lini – Wakili Mwasipu

Tundu Lissu akiwa mahakamani

 

MMOJA wa mawakili wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amesema kuwa hafahamu ni lini kesi ya mteja wake huyo, itarejea tena mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na MwanaHALISI leo Ijumaa, tarehe 28 Novemba, Hekima Mwasipu amesema, “siyo mawakili, wala Lissu mwenyewe, wanaofahamu lini kikao cha mahakama kitakachosikiliza shauri hilo, kitaitishwa.”

Mwenyekiti wa Chadema, yuko kwenye kuta za magereza, tangu Aprili mwaka huu. Anatuhumiwa kwa uhaini.

Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, inayosikiliza shauri hilo lilipoewa Na. 19605/ 2025, ilihairisha kesi hiyo, tarehe 12 Novemba 2025, kwa maelezo kwamba muda uliowekwa na Msajili, umemalizika.

Kabla ya kuhairishwa kwa shauri hilo, Lissu alikuwa amewasilisha mahakamani hapo, hoja sita kupinga sheria ya mashahidi wa siri, akidai kuwa sheria hiyo ni batili, kwa kuwa haijatangazwa kwenye Gazeti la Serikali (GN).

Upande wa Jamhuri uliomba ahirisho ili upate muda wa kujibu hoja hizo.

Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini, linalodaiwa kutendwa kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha sheria ya kanuni ya adhabu, linalotokana na maneno aliyotamka kuhusiana na kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa Hekima, kesi za Mahakama Kuu zinaendeshwa kwa vikao, utaratibu ambao mawakili wengi wamekuwa wakiupinga kwa kuwa unasababisha ucheleweshaji wa mashauri.

Amesema, utaratibu huo unachukuliwa kuwa una muadhibu mtuhumiwa kabla ya kutiwa hatiani jambo ambalo linaathiri haki.

Tangu kesi hiyo ihairishwe, leo ni siku 17; Jamhuri ilikuwa imemleta mahakamani hapo shahidi wake wa siri aliyepewa jina la ‘P1’, ambaye kabla hajaanza kutoa Ushahidi, Lissu alipinga kufuchwa kwake.

About The Author

error: Content is protected !!