November 26, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Rais wa zamani wa Brazil, anaanza maisha mapaya gerezani

Jair Bolsonaro

 

RAIS wa zamani wa Brazil, Jair Bolsonaro, jana Jumanne, alianza kutumikia kifungo chake cha miaka 27 gerezani. Amepatikana na hatia ya kuongoza jaribio la mapinduzi. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Jaji wa Mahakama Kuu, Alexandre de Moraes, aliyeongoza kesi hiyo aliagiza Bolsonaro kubaki kizuizini baada ya kukamatwa Jumamosi iliyopita.

Bolsonaro hatakaribiana na wafungwa wengine wachache wanaozuiwa katika makao makuu ya polisi ya shirikisho.

Jaji De Moraes alichukua uamuzi huo baada ya upande wa utetezi kumaliza rufaa zake.

Mawakili wa Bolsonaro wameahidi kuwasilisha maombi ya kifungo cha nyumbani, kutokana na afya mbaya ya kiongozi huyo wa zamani.

Bolsonaro alitiwa hatiani kwa kula njama ya kuendelea kubaki madarakani baada ya kupoteza uchaguzi wa mwaka 2022 kwa hasimu wake wa siasa za mrengo wa kushoto, Luiz Inacio Lula da Silva, rais wa sasa wa taifa hilo.

Bolsonaro – mshirika mkubwa wa rais wa Marekani, Donald Trump – alikamatwa  katika makazi yake huko Brasília, ili kumzuia kutoroka, siku chache kabla ya kuanza kifungo chake.

Mawakili wake, waliapa kukata rufaa dhidi ya kukamatwa kwake na kutupilia mbali madai kwamba rais huyo wa zamani alikuwa akijaribu kutoroka.

Mtoto wa Bolsonaro, Flávio Bolsonaro, alikuwa ametoa wito kwa watu kufanya mgomo badala ya kukaa nyumbani na kutazama kila kitu kikitokea kwenye simu zao.

Kabla ya kukamatwa Bolsonaro alikuwa katika kifungo cha nyumbani.

Mahakama imeamuru washirika wengine wa Bolsonaro waliopatikana na hatia kuanza kutumikia vifungo vyao. Washirika hao, ni Augusto Heleno, aliyekuwa Jenerali na waziri wa usalama wa taifa.

Amehukumiwa kifungo cha miaka 21; Paulo Sérgio Nogueira de Oliveira, Jenerali na Waziri wa zamani wa Ulinzi, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 19 na Walter Braga Netto, Jenerali na Waziri wa zamani wa Ulinzi, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 26.

Wengine, ni Almir Garnier Santos, Mkuu wa Jeshi la Wanamaji, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 24; Anderson Torres, Waziri wa zamani wa Haki na Usalama wa Ndani, aliyehukumiwa kiungo cha miaka 24; Alexandre Ramagem, Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Brazil (ABIN), aliyehukumiwa miaka 16 na Mauro Cid, msaidizi wa karibu wa Bolsonaro, aliyehukumiwa kifungo cha miaka miwili gerezani.

Majaji wa Mahakama Kuu walisema kwamba Bolsonaro alihusishwa na mpango wa kumuua Rais Lula da Silva na mgombea mwenza Geraldo Alckmin Septemba 2022, pamoja na kumkamata na kumuua Jaji Alexandre de Moraes, aliyekuwa akisimamia kesi zake.

Hata hivyo, mpango huo haukuungwa mkono na makamanda wa jeshi na jeshi la anga, jambo lililowezesha Lula kuapishwa bila matatizo tarehe 1 Januari 2023.

Wiki moja baadaye, maelfu ya wafuasi wa Bolsonaro walivamia majengo ya Serikali mjini Brasilia, na takribani watu 1,500 walikamatwa.

Majaji walibaini kuwa Bolsonaro alichochea vurugu hizo kwa matumaini kwamba jeshi lingemuunga mkono ili aendelee kubaki madarakani.

Mwanasiasa huyo amepigwa ya kugombea nafasi yoyote ya kisiasa hadi mwaka 2060, huku akiitaja kesi hiyo kama “uwindaji dhidi yake” uliolenga kumzuia kugombea urais mwaka 2026.

Bolsonaro sasa ni sehemu ya orodha ndefu ya marais na mawaziri wakuu ambao enzi zao ziliishia kwenye vyumba vya mahakama badala ya majukwaa ya kisiasa.

Wengine waliopitia njia hiyo, ni pamoja na rais wa zamani wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, aliyehukumiwa kwa makosa ya ufisadi.

Kiongozi mwingine aliyeingia matatani, baada ya kuondoka madarakani, ni  na Jacob Zuma, aliyekuwa rais wa Afrika Kusini.

Alikabiliwa na kifungo cha miezi 15 gerezani baada ya kuidharau Mahakama ya Katiba, kutokana na kukataa kuhojiwa kuhusu ufisadi uliodaiwa kutokea wakati wa utawala wake.

Kuingia kwake gerezani kulizua taharuki kubwa nchini Afrika Kusini, lakini alitolewa mapema kwa kile kilichoitwa msamaha wa kiafya, hatua ambayo ilizua maswali kuhusu usawa wa sheria kwa watu wote.

Kwa sasa, Zuma anaishi kwa uhuru katika jimbo la KwaZulu-Natal akiwa na umri wa zaidi ya miaka 80, lakini kesi yake kubwa ya ufisadi katika ununuzi wa silaha bado haijafutwa.

Naye Omar al-Bashir, mtawala wa miaka 30 nchini Sudan, alihukumiwa kifungo cha miaka miwili katika kituo cha uangalizi kwa tuhuma za ufisadi muda mfupi baada ya kung’olewa madarakani.

Kesi yake nzito zaidi inayomkabili, ni ile ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu dhidi ya Binadamu (ICC), inayotaka akabiliane na mashtaka ya mauaji ya Kimbari na uhalifu wa kivita.

Kwa sasa, Bashir anashikiliwa kwenye hospitali ya kijeshi mjini Khartoum kutokana na umri na hali ya nchi yake.

Kesi za ICC bado zimesimama kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na hatma yake imebaki kutegemea utulivu wa kisiasa ambao bado haujarejea nchini Sudan. Orodha ni ndefu:

Kuna Hosni Mubarak, aliyekuwa rais wa Misri. Baada ya kuangushwa kupitia mapinduzi ya Arab Spring, alikabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo mauaji ya waandamanaji na matumizi mabaya ya fedha za umma.

Hatimaye, alihukumiwa miaka mitatu kwa kuidhinisha matumizi haramu ya fedha za serikali kwa ajili ya mali za familia yake, sehemu ya kifungo alichotumikia akiwa hospitalini kutokana na umri mkubwa.

Aliachiliwa mwaka 2017 na kuishi maisha ya utulivu hadi alipofariki 2020.

Tangu wakati huo, mjadala kuhusu urithi wake wa kiutawala umeendelea kugawanya wananchi kati ya waliomuona kama mtulivu aliyeliletea taifa uthabiti na waliomwona kama ishara ya ufisadi wa muda mrefu.

Naye Rais wa zamani wa Korea Kusini, Park Geun-hye, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani, kufuatia kashfa ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Mahakama ilithibitisha ushirikiano wake na rafiki yake wa karibu aliyekuwa akitoa maamuzi ya serikali kwa ushawishi binafsi.

Kesi hiyo ilisababisha maandamano makubwa na kuvuruga hadhi ya taasisi za serikali.

Baada ya kutumikia karibu miaka mitano, Park alipewa msamaha kwa sababu za kiafya. Sasa anaishi kwa faragha jijini Seoul, mbali na utata wa kisiasa uliomwagusha madarakani.

Lee Myung-bak, rais wa 10 wa nchi hiyo pia alihukumiwa miaka 15 kwa ufisadi na kujinufaisha kupitia kampuni aliyoimiliki kwa siri.

Kesi hiyo ilifichua mtandao mpana wa rushwa uliokuwa umejikita kwenye serikali na makampuni makubwa.

Kutokana na umri mkubwa na masuala ya afya, alipewa msamaha wa rais na kwa sasa anaishi kimya jijini Seoul bila nafasi ya kurejea kwenye majukwaa ya siasa.

WaziriMkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan, alihukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani kwa kuvuja siri za serikali na miaka 14 kwa ufisadi.

Ni baada ya mahakama kumhusisha na utumiaji mbaya wa nyaraka za siri na kuchukua mali za serikali kwa maslahi binafsi.

Khan bado yuko gerezani Adiala, huku rufaa zake zikiendelea. Wafuasi wake wanamtaja kama mwathirika wa vita vya kisiasa, lakini uamuzi wa mahakama hadi sasa umesimama pale pale.

Naye Nawaz Sharif – waziri mkuu mwingine wa nchi hiyo – alihukumiwa  miaka 10 kwa kumiliki mali ambazo hakuweza kueleza alizipataje, ikiwemo majengo ya kifahari London.

Ingawa alitumikia muda mfupi, alipewa ruhusa ya kwenda London kwa matibabu ruhusa iliyomruhusu kubaki nje kwa muda mrefu.

Sasa amerudi Pakistan na kuongoza chama chake, lakini kumbukumbu ya hukumu yake bado ni doa linalofuatilia safari yake ya kisiasa.

About The Author

error: Content is protected !!