November 23, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yavikosoa vyombo vya habari vya kimataifa

 

MSEMAJI wa serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amevikosoa vyombo vya habari vya nje akivitaka kufuata maadili na misingi ya uandishi wa habari. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msigwa amevitaja vyombo vya habari vya CNN, Aljazeera, BBC na DW, kwamba vimekuwa vikichapisha habari za upande mmoja zenye nia ovu kwa Tanzania.

“Uandishi wa habari wa aina hii, haukubariki,” alisema Msigwa na kuongeza, “Siyo haki kwa vyombo vya habari kuchapisha habari za upande mmoja na baadaye kusema maafisa wa serikali walipotafutwa hawakupatikana.”

Ametaka kuchapisha taarifa zinazozingatia “usawa, haki na uwajibikaji.”

Msigwa ameitaja CNN kuwa ni chombo kilichokiuka maadili kwa kuchapisha habari zilizojaa ‘tuhuma’ dhidi ya serikali bila kutoa nafasi kwa serikali kujibu.

Aliitaka idhaa hiyo ya Marekani kuwasiliana na serikali kwa lengo la kuchapisha maudhui ya ukweli, akitaja sera ya wanasheria ya ‘principle of natural Justice’ inamaanisha kwamba huwezi kuandika habari za kumtuhumu mtu bila kumpatia mtu huyo fursa kujitetea.

Alisema, “Natoa wito kwa CNN waje upande wa serikali wachapishe maudhui ya ukweli, waache kuchapisha habari za upande mmoja.”

Alisema, “Walichofanya CNN kimefanywa na BBC, DW na Aljazeera.”

Aliongeza kuwa serikali itazungumza na vyombo vya kimataifa ili kuwapatia nafasi ya kujieleza.

Kauli ya Msigwa inajiri kufuatia ripoti za mauaji yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa Tanzania ambao Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi kwa karibia asilimia 98 ya kura.

Bali pamoja na kubinywa kwa mtandao uliovizuia vyombo vya habari nchini humo kuandika taarifa za yale yaliotokea wakati wa uchaguzi huo, vyombo vya kimataifa vilifanikiwa kuandaa taarifa za ghasia hizo za uchaguzi hatua ambayo imezua shutuma kutoka kwa serikali.

Maandamano hayo ya kutaka mabadiliko mbalimbali ikiwemo mifumo ya uchaguzi na usimamizi wa haki, yameelezwa kuwa miongoni mwa machafuko makubwa zaidi nchini Tanzania tangu taifa hilo lipate uhuru wake, tarehe 9 Desemba 1961.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya kimataifa, mamia ya watu wanaripotiwa kufariki dunia.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Mohammed Thabit Kombo, alinukuliwa akisema, serikali haina idadi kamili ya watu waliofariki na uhalibifu ulioyotokea.

About The Author

error: Content is protected !!