November 20, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tukiacha kubaka uchaguzi, tutakuwa salama

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele

 

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametangaza kuunda tume ya kuchunguza matukio ya wakati wa maandamano ya 29 Oktoba, “ili kufahamu” sababisho la maandamano. Anaandika Saed Kubenea, Dar es Salaam … (endelea).

Amesema, taarifa ya tume “ndio itatumika katika mazungumzo ya maridhiano, yenye lengo la kudumisha amani nchini.”

Alitoa kauli hiyo, Ijumaa wiki iliyopita, wakati akifungua Bunge la Jamhuri, mjini Dodoma.

Alisema, amehuzunishwa na mauaji ya raia.

Lakini hakutaja idadi kamili ya waliofariki na hata kujeruhiwa. Ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia majeruhi uponyaji wa haraka.

Swali ambalo wananchi wanajiuliza, ni hili: Rais hafahamu kilichosababisha maandamano? Hafahamu tatizo lilitokea? Tujadili:

Kwanza, kilichosababisha maandamano ya siku ya “uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025,” kinafahamika. Ni kitendo cha walioko madarakani kupuuza kilio cha muda mrefu cha wananchi.

Kwa takribani miaka 30 sasa, wananchi wamekuwa wakitaka kuwapo mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi na ujio wa Katiba Mpya.

Wamekuwa wakitaka viongozi wapatikane kwa njia ya haki. Wametaka tume huru ya uchaguzi; mgombea binafsi, misingi na miiko ya uongozi, Tume ya Haki za Binadamu na maadili ya viongozi wa umma.

Rais Samia Suluhu Hassan

Lakini serikali imepuuza madai hayo na kuamua kubaka uchaguzi, ili kuendelea kusalia madarakani.

Matendo ya kubaka uchaguzi yalianza kushika kasi baada ya uchaguzi mkuu 2015. Mamia ya wagombea upinzani, walioshiriki chaguzi za marudio, kufuatia kujiuzulu kwa waliokuwa wamezishikilia nafasi hizo, kwa madai ya “kuunga mkono juhudi,” wengi walienguliwa.

Baadhi waliambiwa hawajui kusoma na kuandika. Wengine wakadaiwa wamekosea kujazaji wa fomu za uteuzi.

Wachache waliosalia, “walifanyiziwa” siku ya uchaguzi. Mifano ni mingi.

Bali kilichotendeka kwenye chaguzi tatu zilizofuata – uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa 2019 na 2024, pamoja na uchaguzi mkuu 2020 – ndio sababishao kuu la mwitiko wa maandamano.

Hii ni kwa sababu, wananchi wameona chaguzi zao zinavyovurugwa. Wameona na kushuhudia chaguzi zinavyogubikwa na ulaghai na zinazoendeshwa kinyume cha sheria.

Wameona jinsi serikali inayohubiri kulinda haki ya kila mwananchi kujiandikisha na kupigakura, ilivyoshindwa kutekeleza wajibu wake.

Wameona viongozi wao wanajenga msingi mbovu wa kutaka wananchi watii “batili” na kufunika demokrasia kwa blanketi.

Katika mazingira haya, nani anatafuta mchawi wa maandamo ya 29 Oktoba?

Kingine kilichosababisha kuwapo maandamano, ni hatua ya serikali, kunyamazia vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji nchini.

Kwa miaka minne sasa, taifa limegubikwa na vitendo vya utekaji, utesaji na mauaji ya raia. Wananchi wamelalamika kuchukuliwa kwa ndugu na jamaa zao na wanaoitwa na serikali, “watu wasiojulikana.”

Hakuna hatua zilizochukuliwa. Hakuna aliyekamatwa; na au aliyeokolewa kutoka mikononi mwa wasiojulikana.

Badala yake, jeshi la polisi limeendelea kung’anga’na kuwa haiwafahamu wanaohusika na utekaji ambao haukomi; huku wakiwa mikono mitupu bila angalau na ushahidi wa tunda la uchunguzi.

Karibu wote waliotekwa, kuanzia Ben Saanane, Deusdedith Soka, Jacob Mlay, Frank Mbise, Mdude Nyangali, Azory Gwanda, hadi Humphrey Polepole, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba; aliyechukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake, Ununio, jijini Dar es Salaam; hakuna aliyewahi kurudi.

Pili, maandamano ya 29 Oktoba, yametokana na kupuuzwa kwa ripoti ya Tume ya Haki Jinai, iliyoundwa na rais mwenyewe, mwaka 2023 na iliyoongozwa na Jaji Othman Chande.

Tume ya Jaji Chande ilisema, taswira ya jeshi la Polisi imeharibika; kumekuwapo malalamiko ya muda mrefu, juu ya vitendo vinavyochafua taswira ya jeshi hilo.

Wakasema, polisi wameshindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi wananchi, rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio.

Tume ikapendekeza, jeshi liundwe upya na kubadilishwa muundo na fikra; ili kuwa na jeshi lenye taswira ya kuhudumia wananchi.

Mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari, navyo vibadilishwe, kutoka katika dhana ya ujeshi (police force), kwenda dhana ya kuhudumia wananchi. Hakuna kilichofanyiwa kazi.

Vilevile, ripoti ya Kikosi Kazi cha Rais, kilichoongozwa na Prof. Rwekaza Mukandala, pamoja na ahadi ya Rais Samia mwenyewe ya tarehe 6 Mei 2023, kuhusu ujio wa Katiba mpya, havikifanyiwa kazi.

Kikosi kazi kilipendekeza mchakato wa Katiba uliokwama tangu mwaka 2014, kufufuliwa tena. Chama Cha Mapinduzi (CCM), tarehe 22 Juni 2022, kikatangaza kuridhia ufufuaji wa mchakato huo.

Lakini tangu wakati huo, hakuna taarifa yoyote kuhusu jambo hilo. Hakuna aliyeeleza hata matumizi ya Sh. 9 bilioni, zilizotengwa na serikali katika bajeti iliyopita, kuandika katiba mpya jinsi zilivyotumika.

Katika mkutano wa bajeti inayoishia 30 Juni 2024, serikali iliiongezea wizara ya katiba na sheria, mabilioni hayo ya shilingi, ili kukwamua mchakato wa Katiba.

Mchakato wa Katiba mpya ulikwama, baada ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum, kujiondoa bungeni. Walikituhumu chama tawala, kutumia wingi wake bungeni, kuchakachua maoni ya wananchi.

Rais Samia alikuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba. Angetaka taifa kuwa na katiba mpya, kabla ya uchaguzi uliosababisha vifo vya mamia ya wananchi, hasa baada ya kuwa rais, ingepatikana.

Rais anajua kasi ya hoja za katiba mpya; msisitizo wa baadhi ya viongozi wa upinzani na chama chake – wa sasa na wastaafu; mabingwa wa sheria na katiba, wanasiasa na wanaharakati, kutaka kuwapo kwa Katiba mpya.

Ndio maana alisema, “watu wanataka katiba yao.” Alikiri ukweli; ama kwa kusema waziwazi au kwa vitendo.

Hii ni kwa sababu, chimbuko la matatizo yanayolikabili taifa hili, yanatokana na chama kilichopo Ikulu kujiingiza kuwa sehemu ya Katiba ya Jamhuri kupitia Katiba ya muda ya mwaka 1965 na katiba ya kudumu yam waka 1977.

Ndani ya Katiba hizi mbili, CCM imejiona ni kubwa kuliko wananchi. Hilo halijaweza kubadilika hata sasa, tunapofuata mfumo wa vyama vingi. Kinachoonekana kuwa mabadiliko, ni geresha tu.

Katiba inataja mihimili mikuu mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali. Lakini Katiba inampa mamlaka rais kuteua mawaziri, kutoka miongoni mwa wabunge.

Wakati haya yanafanyika, Katiba hiyo hiyo, inasisitiza kuwa “Bunge ni chombo kikuu cha wananchi.” Bunge ambalo limeingiliwa na serikali, haliwezi kuwa Bunge la wananchi. Hiki ni chombo cha rais.

Katiba inamtaja rais kuwa sehemu ya Bunge. Hii maana yake ni kwamba Bunge linawajibika kwa rais; hata katibu wa Bunge, tumeshuhudia akiteuliwa na rais.

Naye mkuu wa mkoa au wilaya – kama ilivyokuwa wakati wa chama kimoja – walipovalishwa kofia ya chama, serikali na Bunge, wanaendelea hivyo mpaka sasa.

Kwa mfano, Amos Makalla, alikuwa katibu mwenezi wa CCM. Leo mkuu wa mkoa wa Arusha. Kwa nafasi yake hiyo, ni mjumbe wa Kamati ya siasa ya mkoa, huku akiwa anasimamia watendaji wa serikali, wakiwamo wakurugenzi wa halmashauri, miji, manispaa na majiji.

Kipyenga cha uchaguzi kinapopulizwa, wakurugenzi hao, ndio hugeuza kuwa wasimamizi wa uchaguzi. Wala mfumo wa vyama vingi haujamuondolea rais kofia yake ya uenyekiti wa chama.

Ndio maana aweza kuteua mkuu wa mkoa akampa majukumu ya kiserikali, kisha akamhamishia kwenye chama au Bunge.

Tatu, Ibara ya 14 ya Katiba, inatoa haki ya kuishi kwa kila raia; na kupata kutoka katika jamii, hifadhi ya maisha yake.

Kwa tafsiri ya haraka, ni kwamba kila mtu anayo haki ya kuishi; na maisha yake yanapaswa kulindwa na serikali.

Kwamba, taifa hili linafuata misingi ya demokrasia na haki ya jamii, ambapo wananchi ndio msingi wa mamlaka na serikali hupata madaraka na mamlaka yake, kutoka kwa wananchi.

Ukisoma kwa umakini Ibara hiyo ya Katiba, utabaini kuwa wananchi ndio chanzo cha madaraka na mamlaka. Ndiyo sababu, wanachagua viongozi wao.

Hivyo pale inapotekea, waliopewa jukumu la kulinda uhai wa raia, wanashindwa kutimiza jukumu hilo; na kuishia kufyatulia risasi za moto wanaopaswa kulindwa, huo ni ukiukaji wa Katiba.

Hatua ya rais ya kutokemea maofisa wa polisi waliowashambulia raia kwa risasi hadi majumbani na kuwajibisha, hakuwezi kusaidia kutatua tatizo.

Hata kule Rais kutozungumzia vitendo vya utekaji na utesaji; kutojadili malalamiko ya wananchi kuhusu kuzuiliwa kwa miili ya waliouawa kwenye maandamano, kunaweza kutafsriwa kuwa anabariki kilichotendeka.

Wapo wanaosema, walifikisha miili ya wapendwa wao hospitalini na kulipia sehemu ya gharama za kuhifadhi mwili na kupewa lisiti. Lakini walipokwenda kuzichukua kwa ajili ya mazishi, hawakuweza kuzipata.

Mpaka hapo, bado Rais anaona kuna umuhimu wa kuunda tume ya uchunguzi?

Watu wote wanaolitakia mema taifa hili, walishasisitiza umuhimu wa kuwapo maridhiano kabla ya uchaguzi.

Waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba na baadhi viongozi wa madhehebu ya kidini, walilieleza hili vizuri, lakini hawakusikilizwa.

Kuna waliodiriki hata kupiga magoti kuomba serikali isikilize kilio cha wananchi.

Wengine wakakumbusha hadi 4R za Rais – Maridhiano, Uthabiti, Mageuzi na Kujenga upya – lakini wakaishia kujibiwa, “hazimaanishi kuwa na serikali kibogoyo.”

Kanisa Katoliki likaeleza juu ya umuhimu wa mabadiliko ya Katiba, ili kuwa na uchaguzi huru na haki, lakini wakaishia kushambuliwa kwa katibu mkuu wao, Padre Charles Kitima.

Askofu Gwajima alipojitokeza kupinga utekaji na madaraka makubwa ya rais, Kanisa la Ufufuo na Uzima, ambalo yeye ni kiongozi wake, likapigwa komeo. Orodha ni ndefu.

Tuache kuwa nchi ya ripoti na maneno mengi. Wananchi wanataka vitendo. Maumivu waliyopata hayawezi kuponywa kwa kauli za kisiasa; yaweza kuponywa kwa matendo ya dhati – ya kiutu na haki.

Tukiacha kupora mamlaka na madaraka ya wananchi kwa njia ya wizi wa kura; tukarudi kwenye mstari kwa kufanya chaguzi huru na haki, tutatoka kwenye mkwamo huu.

Tume za Jaji Joseph Sinde Warioba, Jaji Francis Nyalali na nyingine, tayari zimeweka msingi wa maridhiano ya kudumu. Tutekeleze kilichopendekezwa.

About The Author

error: Content is protected !!