Rais Samia Suluhu Hassan
RAIS Samia Suluhu Hassani amesema kwa maandamano na vurugu zilizotokea tarehe 29 Oktoba 2025 siku ya Uchaguzi mkuu yameitia doa nchi na kuiweka Tanzania kwenye wakati mgumu ya kupata mabilioni za mikopo na ufadhili kutoka kwa wahisani na wafadhili. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Maandamano hayo ya kudai haki na kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu yalitokea kwenye mikoa mbalimbali yalisababisha uharibifu wa mali za umma, binafsi, vifo na majeruhi waliopigwa risasi zilizokuwa zikirushwa holela na askari waliokuwa wakidhibiti.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo, tarehe 18 Novemba 2025 jijini Dodoma katika hafla ya kuwaapisha mawaziri na manaibu mawaziri aliowateua jana ambapo aliwataka wakafanye jukumu la kusaka fedha kutoka vyanzo vya ndani.
Amesema kuwa kilichotokea siku ya uchaguzi kimelipunguzia taifa sifa ya kupata mikopo au ufadhili kutoka kibenki na taasisi za kifedha za kimataifa hivyo kuna uwezekano wa kurudi nyuma.
“Mara nyingi tunategemea kupata mikopo kutoka nje, mikopo kutoka taasisi mbalimbali, benki za kimataifa, lakini yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza tulikuwa tunapata sana kwa sifa zetu, kwa kazi tulizokuwa tunazifanya
“Doa tulilojitia huenda likaturudisha nyuma kwa maana hiyo tuna kazi ya kutafuta fedha humu ndani kupitia rasilimali zetu alizotupa Mungu, tutaangalia njia gani ya kutupa fedha ili tukatekeleze miradi tuliyopanga kuitekeleza,”- Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha Rais Samia amesema hatachoka kubadilisha baraza la mawaziri mpaka pale atakapopata mtu sahihi wa kufanya kazi kwa moyo mmoja na kuwataka mawaziri kuwajibika kwa wananchi na kutekeleza yale yote waliyoyaahidi.
Amewataka mawaziri hao kubeba majukumu ya kuwatumikia wananchi na waishi kwenye kauli mbiu yao ya ‘Kazi na Utu’ kwa kuheshimu utu wa Mtanzania.
ZINAZOFANANA
Mwanajeshi wa Marekani akamatwa na mabomu Tanzania
Machafuko ya 29 Oktoba: Maaskofu Katoliki wataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wawajibike
Shinikizo la kufanyika uchunguzi wa mauaji ya 29 Oktoba lashika kasi