November 13, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Tuache kiburi, tuliokoe taifa – Mwabukusi

Boniface Mwabukusi

 

RAIS wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, amewataka viongozi wa serikali kuacha kiburi, ili kuliokoa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

“Ni muhimu kwa watawala kuacha kiburi na kuwasikiliza wananchi,” ameeleza mwanasheria huyo mahiri nchini. Amesema, “…hali hii haihitaji kiburi.”

Amesema, wanachotaka wananchi kwa sasa, ni vitu vitatu – ukweli, haki na uwajibikaji na kuongeza, “hayo ndio mambo yatakayotusaidia kutoka kwenye hali tuliyonayo sasa.”

Mwabukusi ametoa kauli hiyo, leo tarehe 13 Novemba 2025, nje ya kituo kikuu cha Polisi cha Kati (Polisi Centro), jijini Dar es Salaam, alipokwenda kumsindikiza Mpale Mpoki, mwanachama wa TLS, aliyekwenda kwenye kituo hicho, kuitikia wito wa polisi.

Amesema, watawala waache kuwalaumu vijana, kwa walichokifanya, badala yake, tuilaumu mifumo yetu ili iweze kuleta uwajibikaji.

Aidha, Rais wa TLS, amelitaka jeshi la polisi kukabidhi miili ya watu wote waliopoteza maisha kwenye maandamano ya 29 Oktoba.

Amesema, ni muhimu kwa miili ya watu waliouawa kwenye vurugu za uchaguzi, wakarudishwa kwa ndugu zao ili waweze kupewa heshima na kuongeza, “jeshi la polisi liache kukamata watu hovyo.”

Machafuko ya uchaguzi yaliyopoteza uhai wa mamia ya wananchi, yamechochewa na kasi ndogo ya mageuzi kwenye mifumo ya uchaguzi nchini.

Uchaguzi huo, uligubikwa na vurugu, milio ya risasi, majeruhi na misiba iliyofuata – katika nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa kimbilio la wakimbizi.

About The Author

error: Content is protected !!