Spika Mussa Azzan Zungu
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu, ametangaza kuwa kesho tarehe 13 Novemba 2025, Bunge la 13 katika Mkutano wa Kwanza, Kikao cha Tatu, litakuwa na shughuli muhimu ya kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sambamba na uchaguzi na uapisho wa Naibu Spika wa Bunge. Anaripoti Zakia Nanga, Dar es Salaam … (endelea).
Zungu ametoa kauli hiyo leo, tarehe 12 Novemba 2025, wakati akiahirisha kikao cha pili cha Bunge, Jijini Dodoma. Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wabunge wote kuhudhuria kikao hicho bila kukosa, kutokana na uzito wa ajenda zilizopangwa kujadiliwa.
Ikumbukwe kuwa Bunge hili la 13 lilianza Jumanne, tarehe 11 Novemba 2025, likianza na uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kisha kiapo cha uaminifu na ahadi ya uzalendo kwa wabunge wateule, zoezi ambalo limehitimishwa siku ya leo.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ilivyorekebishwa), uteuzi wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hufanyika kwa kufuata utaratibu maalum unaoanza mara baada ya Rais kuapishwa rasmi kushika madaraka.
Ibara ya 51(1) ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya kumteua Waziri Mkuu, ambapo mteule lazima awe Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katiba inaeleza kuwa uteuzi huo unapaswa kufanyika ndani ya siku kumi na nne (14) tangu Rais kuapishwa, na mteule anatakiwa kuwa Mbunge kutoka chama chenye wabunge wengi zaidi bungeni, au ikiwa hakuna chama chenye wingi, basi awe Mbunge anayekubalika na wabunge wengi.
Baada ya uteuzi huo, jina la Waziri Mkuu mteule hupelekwa Bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kupitia Azimio la Bunge litakaloungwa mkono na kura nyingi za wabunge waliohudhuria kikao. Mteule atathibitishwa rasmi endapo atapata uungwaji mkono wa wabunge wengi.
Mara baada ya kuthibitishwa, Waziri Mkuu hula kiapo cha uaminifu na ahadi ya uadilifu mbele ya Rais au mtu aliyeidhinishwa naye, ndipo kuanza rasmi kutekeleza majukumu yake.
Kwa mujibu wa Ibara ya 52 ya Katiba, Waziri Mkuu ndiye Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni na husimamia utekelezaji wa sera na shughuli za Serikali ya Muungano kwa niaba ya Rais.
ZINAZOFANANA
Ngoma bado mbichi, Lissu aibuka na pingamizi jipya
Lissu apinga shahidi wa siri kutoonekana na majaji
Hatujatolewa kwa sababu ya maridhiano -Heche