Othman Masoud Othman
HUKU akijinasibu kuwa kimahesabu Chama cha ACT Wazalendo kitapata ushindi mkubwa usiowahi kutokea, Mwenyekiti wake, Othman Masoud Othman, ameasa mamlaka zinazohusika na jukumu la ulinzi na usalama kuchukua hatua madhubuti
kuzuia njama za kuhujumu uchaguzi wa Zanzibar. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano alouandaa leo Hoteli ya Golden Tulip ya Uwanja wa Ndege Zanzibar, Othman alisema pamoja na mipango yote iliyoandaliwa ya kuvuruga uchaguzi, “labda kutumike nguvu isiyo ya kawaida
kubadilisha kiu ya wananchi kukiondoa madarakani Chama Cha Mapinduzi {CCM}.”
Othman, Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameeleza masikitiko yao kwamba Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar {ZEC}, inatumiwa na CCM kusimamia mipango ya kuvuruga uchaguzi pamoja na kutambua wazi wajibu wa kikatiba ilionao wa kuhakikisha inaendesha uchaguzi kwa kufuata sheria na taratibu zake.
“Kwa mfano hii kura ya mapema ambayo kwa kweli ni wizi wa mapema tumeona hata hiyo idadi ya walotajwa kushiriki inazidi idadi ya hao wanaotambuliwa na sheria hiyo ya kihuni. Kuna makada wa CCM, wageni, wapo wagombea wa vyama, wapo hata maiti. Na orodha ya watakaoshiriki haikuwekwa na picha zao. Lakini tunajua pia mpango wa kuwatoa nje mawakala
wetu.
“Hawa baada ya ukiukaji mkubwa wa utaratibu wa kuteua wasimamizi wa uchaguzi, wengine wakipewa taarifa bila ya kuomba kazi ya usimamizi wakighushi taarifa za hao waliowateua ionekane mtu ni mwalimu kumbe ni askari wa vikosi. Mpaka kufikia
kujipangia majimbo ya kuyachukua kwa nguvu… tunajua wakati huu wanayo matokeo yao mkononi ya kuja kuyatangaza watakaposhindwa kama tunavyotarajia.
“Ndo maana tunasema Tume inashirikiana na CCM kuvuruga uchaguzi. Bado tunasema pamoja na yote hayo wanayoyapanga kwa kuitumia Tume, tunaenda kuthibitisha ushindi mkubwa wa ACT Wazalendo ambao haujawahi kutokea katika historia ya mfumo wa vyama vingi ulioanza mwaka 1992. Tunasihi mamlaka husika zichukue hatua kuzuia njama za kuvuruga uchaguzi huu,” alisema.
Othman akigusia hatua yao ya kuiandikia Tume ya Uchaguzi Zanzibar kuhusu matatizo mbalimbali waliyoyaona ya kasoro kwenye usimamiaji uchaguzi, alisema Tume haijatoa majibu mpaka muda anazungumza na waandishi wa habari.
“Hawajajibu lolote lakini msimamo wetu ni kwamba tumechukua kila jitihada na kumfikia kila anayestahili kuyaeleza mambo haya na kusihi kuwa wananchi hawatarajii kushuhudia dhulma dhidi ya maamuzi yao kwenye sanduku la kura. Wala haiwezekani nchi kufanywa kama iliyo vitani wakati uchaguzi ndio njia ya kidemokrasia ya wananchi kupata viongozi wanaowataka kusimamia majambo yao. Mengine tunaendelea kuyafanyia kazi lakini tunasema lazima ifike mahali wenzetu wafikirie maslahi makubwa ya nchi na watu wake,” alisema.
Kuhusu mwenendo wa kampeni ya uchaguzi iliyoanza tarehe 12 Agosti, Othman alisema kipindi hicho haikuwa tu nafasi kwao kueleza sera zao, bali wameongezewa ujuzi, maarifa na mikakati ya utekelezaji kutoka kwa wananchi.
“Tumegundua kuguswa mno na kero nyingi za wananchi zaidi ya tulivyojua. Tumetambua mgogoro mbaya kabisa wa ardhi unaoliua taifa letu. Chanzo kikuu ni kutofuatwa sheria na taratibu za nchi na baadhi ya watu kutumia vibaya nafasi zao katika utumishi wa umma. Tumeelezwa adha za hospitali zisizo na huduma bora na bima ya afya isiyokuwa na tija. Tumeshuhudia mfumo wa elimu unaoendeshwa kisiasa zaidi huku heshima na hali ya maisha ya mwalimu ikiwa duni sana.
Tumesikia kero kubwa za wavuvi, wakulima wasiokuwa na soko. Tumejionea jinsi raia wanavyonyimwa haki za kimsingi kama vile vitambulisho na vyeti vya kuzaliwa, kero za wafanyabiashara waagiziaji bidhaa wanazopata kutokana na kudorora kwa huduma za Bandari kiasi cha kusababisha baadhi yao kufilisika na wengine kupata hasara kubwa.
“Mengi mengine yaliyokuwa sauti ya Wazanzibari ikiomboleza jinsi Zanzibar yetu ilivyo na udhaifu mkubwa kwenye utawala, utoaji haki, na huduma za kijamii. Mustakabali wake unatishiwa, na matumaini yao kwetu sisi ACT Wazalendo kuja kuiokoa kutokana na maono na sera tulizozibainisha kwao,” alisema.
Uchaguzi mkuu unaokusudiwa kuipatia nchi Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar, unaanza kesho kwa kura ya mapema ambayo imekuwa ikipingwa kwamba ni kinyume na Katiba ya Zanzibar.
Wananchi walio wengi, ukiacha walioidhinishwa na kifungu 81 cha Sheria ya Uchaguzi Namb. 4 ya Zanzibar ya mwaka 2018, watapiga kura zao Jumatano. Mbali na kura hizo tatu, Wazanzibari wanapiga kura mbili – ya kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mbunge.
Othman alihutubia mkutano huo akiambatana na viongozi waandamizi wa chama akiwemo Makamo Mwenyekiti Ismail Jussa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Timu ya Ushindi pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama.
ZINAZOFANANA
Chadema yaja na orodha mpya ya waliotekwa
Chadema yataka Heche achiwe huru
Hatuna mawakala, kura zitalindwa na INEC