
Tundu Lissu akiwa mahakamani
KESI ya uhaini, inayomkabili Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imezidi kunoga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akizungumza mahakamani leo Jumatatu, tarehe 20 Oktoba 2025, Lissu alisisitiza kuwa video inayotakiwa kutolewa na shahidi wa tatu wa serikali, hakuionyeshwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Anasema, “Hiyo video haikuonyeshwa Kisutu. Waheshimiwa majaji, wanataka kuileta hapa, haiwezekani. Naomba muwakatalie,” alieleza na kuongeza, “Ni lazima kesi iendeshwe kwa mujibu wa sheria.”
Lissu alitoa kuali hiyo, wakati akijibu hoja za upande wa mashitaka, kufuatia maelezo ya Nassoro Katuga, Wakili Mkuu wa Serikali, aliyedai kuwa video hiyo, ilionyeshwa na upande wa Jamhuri.
Alisema, “Naomba ikumbukwe kuwa huyu shahidi ni mtaalaamu na kwenye ushahidi wake aliandikiwa barua na vielelezo vililetwa kwa maandishi afanye uchunguzi wa hivyo vielelezo.
“Hizo barua hazijawasilishwa. Anasema, amesaini dispachi, lakini haijaletwa hapa mahakamani. Anasema alivituma hivyo vielezo kwa requesting authority, lakini hajasema vimerudije kwake tena.”
Lissu aliiambia Mahakama Kuu, kwamba waendesha mashitaka pamoja na shahidi wao, wamefanya mambo kienyeji na mambo ya kienyeji hayakubaliwi mahakamani.
Akizungumza kilichojadiliwa, Lissu alisema, “…nitamkumbusha maneno yake Wakili wa Serikali kuwa alisema Mahakama hii sio ya mama yangu na mimi namwambia leo kuwa Mahama hii siyo ya mama yake Katuga wala mama wa huyu shahidi.”
Akasimama Katuga na kusema, “Waheshimiwa majaji, mahakama hii sio ya mama yetu wote.” Lissu akajibu: “…ni sawa. Mahakama hii sio ya mama yetu sote na usifanye mambo kama uko kwa mama yako.”
Baada ya mabishano hayo ya kisheria, kesi imehairishwa hadi Jumatano, tarehe 22/10/2025 saa tatu asubuhi, kwa ajili ya kutolea uamuzi pingamizi lililowasilishwa na Lissu dhidi ya kielelezo ambacho upande wa mashitaka unataka kipokelewe mahakamani.
ZINAZOFANANA
Mageuzi ya uchumi na fedha yamejenga Z’bar shirikishi
Sina hofu yoyote ushindi ninao – OMO
Wassira ataja sababu za Watanzania kumpa mitano Samia